Wakala wa Vipimo yaanza kuweka stika maalum katika vipimo mbali mbali vitakavyo hakikiwa

Imewekwa:January 09, 2017

Katika jitihada za kuboresha zaidi na kwenda na teknolojia ya kisasa ya kumlinda mlaji katika vipimo, Wakala wa Vipimo (WMA) kwa mwaka huu (2017) itaanza rasmi uwekaji wa sticker katika vipimo vya aina mbalimbali.

1. Uwekaji wa Sticker katika pampu za kuuzia mafuta

Kwa mwaka 2017 itaanza rasmi kubandika sticker kwenye pampu zinazotumika katika vituo vyote vya mafuta tutakavyovihakiki, ili mteja ajue uhalali wa kipimo hicho cha mafuta. Kwani mteja ataona sticker itakayodhihirisha kituo hicho kimehakikiwa na Wakala wa Vipimo.

2. Kwenye Bohari za Mafuta (Flow Meters)

Wakala wa Vipimo pia itaweka sticker maalumu katika flow meters zinazotumika kujaza mafuta katika magari ya kubebea mafuta, hivyo wabebaji wa mafuta kwa magari wataweza kutambua flow meter iliyohakikiwa.

3. Mizani za Barabarani (Weigh Bridge)

Katika jitihada za kumlinda mlaji, Wakala wa Vipimo huwa inahakiki mizani zote za barabarani ili kujua kama mizani hizo zinapima kwa usahihi,

Kwa mwaka 2017 na kuendelea, kila mzani wa barabarani utakaohakikiwa na Wakala wa Vipimo utawekewa sticker maalumu ili muhusika wa gari aweze kutambua mzani uliohakikiwa.

4. Mizani za wafanyabiashara na mizani zinazotumika viwandani

Mizani yote ya wafanyabiashara pia uhakikiwa ili kujua usahihi wake.

Aidha, Wakala wa Vipimo awali tulikuwa tunahakiki mizani na kugonga mhuri wa Serikali katika mawe na mizani zote za wafanyabiashara na mizani zinazotumika katika viwanda kwa ajili ya ufungashwaji wa bidhaa, hivyo: kwasasa tutaboresha zaidi, mizani zote zitakazohakikiwa zitagongwa mhuri pamoja na kubandikwa sticker ambayo itakuwa rahisi kuonekana.

5. Mizani za Kuuzia Mazao ya Wakulima

Katika jitihada za kumlinda mkulima na mfanyabiashara pia, Wakala wa Vipimo uhakiki mizani hizo za kupimia mazao ya wakulima (kama vile mazao ya korosho, pamba, ufuta n.k)

Awali mizani hizo zilikuwa zinagongwa mhuri wa serikali tu, ila kuanzia January 2017, kwa kila mzani utakaohakikiwa utagongwa mhuri wa Serikali pamoja na kubandikwa sticker maalumu kutoka Wakala wa Vipimo.

DHUMUNI LA KUANZISHA UBANDIKAJI WA STICKER KATIKA MAENEO TAJWA

- Kwa mlaji itamsaidia kujua uhalali wa kipimo husika, kwani baada ya kubandika sticker na Wakala wa Vipimo mlaji atajiridhisha kuwa mizani anayopimiwa bidhaa au kituo cha mafuta anachohudumiwa kimehakikiwa na mamlaka husika (Wakala wa Vipimo)

FAIDA

- Inasaidia kujua ujazo sahihi wa gari husika linalosafirisha mafuta, mchanga/ kokoto

- Husaidia walaji kujua kama kipimo kimehakikiwa au hakijahakikiwa.

WITO

Tunatoa wito kwa wafanyabiashara wote wanaotumia vipimo, kuhakikisha vipimo vyao vimehakikiwa na Wakala wa Vipimo na kuwekewa sticker stahiki,

Sticker hazifanani (kila sticker ina jina lake kulingana na kipimo) na kila kipimo kina sticker yake.