Elimu kuhusu matumizi sahihi ya Vipimo na Ufungashaji Mkoa wa Njombe
Imewekwa:September 29, 2021
WAKALA WA VIPIMO YASISITIZA MATUMIZI YA VIPIMO SAHIHI MKOANI NJOMBE
Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Marwa Rubirya ameipongeza
taasisi ya Wakala wa Vipimo kwa uamuzi wa kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya
Vipimo na ufungashaji kwa Wakulima na viongozi mbalimbali wa Serikali kwani
madalali Mkoani Njombe wamekuwa na tabia ya kuwanyonya wakulima kwa
kuwalazimisha kununua mazao yao mashambani kwa kutumia Vipimo batili kama ndoo
na Lumbesa.
Mhe, Rubirya amesema elimu ya Vipimo itasaidia
Wakulima kuuza mazao ya kwa kutumia Vipimo sahihi vilivyohakikiwa ili mkulima
aweze kunufaika kwa kupata fedha inayolingana na thamani ya mazao yake na
kutaka vianzishwe vituo maalum kwa ajili ya kuuzia mazao na viewe na mizani
iliyohakikiwa. Pia, ameitaka Wakala wa Vipimo kwa kushirikiana na taasisi
zingine kukaa pamoja na kuhakikisha wanatoka na vifungashio ambavyo
vinakubalika kwa nchi nzima hii itasaidia mazao yatakapofika sokoni yote kuwa
na thamani sawa na ushindani utakao fanana kwenye soko.
Akizungumza na Mwandisi wetu Mhe. Balozi Dk. Pindi
Chana Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Njombe ambaye Ofisi yake imeshirikiana na
Wakala wa Vipimo kutoa mafunzo kuhusu matumizi sahihi ya Vipimo na Ufungashaji
kwa Wakulima amesema, mpaka sasa Elimu ya Vipimo imetolewa katika Wilaya tatu
ambazo ni Njombe Mjini, Wanging,ombe na Makete ambapo jumla ya Wajasiriamali na
Wafanyabiashara 400 wamenufaika kwa kupata elimu kuhusu vipimo sahihi na namna
ya kutambua kipimo kilicho hakikiwa.
Balozi Pindi chana amesema, elimu hii imekuja kipindi
sahihi kwani suala la vipimo limekuwa changamoto hasa katika Mkoa wa Njombe
ambapo Wananchi wanajihusisha na Kilimo cha Mahindi, Maharage, Parachihi na
Viazi Mkulima analima kwa tabu kwa kutumia gharama kubwa lakini wanapokuja
madalali kununua mazao wanalazimisha kununua kwa Vipimo batili vya Lumbesa na
Visado hali inayosababisha mkulima kupata faida kidogo tofauti na ambavyo
angeuza katika mzani angepata faida kubwa ndio maana tumeona kunahaja wakulima
wapate elimu ya Vipimo na kufahamu faida za kuuza kwa kutumia mizani.
Kwa upande Wake Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa
Njombe Bw.Hennry Msambila amesema Wakala wa Vipimo hufanya uhakiki wa Vipimo
mbalimbali katika Mkoa wa Njombe na mara baada ya ukaguzi mkuu hufanya kaguzi
za kushtukiza katika maeneo mbalimbali ili kujiridhisha kama Vipimo hivyo
vinatumika kwa usahihi kama vilivyohakikiwa awali. Pia, katika kuhakikisha
Mkulima analindwa na kuuza mazao yake kwa kutumia Vipimo sahihi amehimiza
Halmashauri zote kuhakikisha zinaanzisha maeneo maalumu ya kuuzia mazao na
kuhakikisha wanaweka mizani iliyohakikiwa ili kuwasaidia Wakulima kuuza mazao
yao kwa kutumia mizani hali ambayo itawasaidia Wakulima kupata fedha nyingi
zitazoendana na mazao wanayouza.
Meneja Msambila amesema, Wakulima wanaouza mazao yao
mashambani kwa kutumia vipimo batili wanaikosesha mapato Serikali na
Halmashauri kwa kuto kukusanya ushuru halisi unaopaswa kulipwa. Vilevile
amesema ufungashaji batili wa mazao kwa mtindo wa Lumbesa unadhohofisha ata
afya za vibarua wanaokuwa wanabeba mizigo hiyo ambayo inakuwa na uzito mkubwa
kinyume na Sheria ya Vipimo inavyoagiza.
Bi. Salome Benald ambaye ni Mkulima Wilaya ya
Wanging’ombe ameeleza kuwa elimu aliyoipata kuhusu matumizi sahihi ya Vipimo na
Ufungashaji imewafumbua sana macho watahakikisha wanawafikishia na wenzao ili
wasiuze tena mazao yao kwa kutumia vipimo batili kama Lumbesa na Visado bali wajikusanye
na kununua mizani zitakazo wasaidia kuuza mazao yao kwa kilogramu ili waweze
kunufaika na mazao wanayolima kuliko kuwanufaisha Wafanyabiashara.