Elimu kuhusu matumizi sahihi ya Vipimo na Ufungashaji kwenye Maonesho ya SIDO Kigoma
Imewekwa:September 30, 2021
UMUHIMU WA KUTUMIA VIPIMO SAHIHI KWA BIDHAA ZA WAJASIRIAMALI
Wakala wa Vipimo Mkoa wa Kigoma ni miongoni mwa
taasisi za Serikali zinazoshiriki katika Maonesho ya tatu ya SIDO Kitaifa
ambayo yanafanyika katika Viwanja vya Umoja Kasulu Mkoani Kigoma. Meneja wa
Wakala wa Vipimo Kigoma Bw. Laurent Kabikiye ameeleza kuwa, maonesho ya SIDO
yamekuja kwa wakati muhafaka kwani yanatoa fursa ya Wajasiriamali wengi
kukutana na taasisi mbalimbali za Serikali na kutatua changamoto zao.
Meneja Kabikiye amesema, Wajasiriamali wengi
wanachangamoto katika uwekaji alama kwenye vifungashio vyao hivyo maonesho haya
yamewawezesha Wakala wa Vipimo kukutana na Wajasiriamali zaidi ya 100 na kuwapa
elimu kuhusu matumizi sahihi ya Vipimo na namna ya kuandika alama za Vipimo kwa
usahihi ili kuongeza thamani ya bidhaa zao ziweze kushindana katika masoko ya
Kimataifa.
Makosa mbalimbali yaliobainika katika ufungashaji wa
bidhaa za wajasiriamali na kupatiwa ufumbuzi ni pamoja na wafungashaji wa
bidhaa za asali baadhi yao wamefungasha bidhaa zao kwa ujazo wakati kwa mujibu
wa Sheria ya Vipimo asali ni nzito inapaswa kufungashwa kwa uzito. Hivyo,
wajasiriamali wamepatiwa elimu hiyo na wameahidi kubadilisha ufungashaji wa
bidhaa za asali na kufungasha kama Sheria inavyoelekeza.
Makosa mengine ambayo wajasiriamali wameelimishwa
kutoyarudia kwenye vifungashio vyao ni pamoja na uandishi wa alama mbalimbali
ambapo baadhi ya wajasiriamali hukosea kuandika alama hizo kama zilivyo
orodheshwa; KGM, kgs, GRM, ML, lts, LTS, CM, Mm. Alama sahihi za Vipimo
huandikwa kwa usahihi mfano kilogram (kg), gram (g), metre (m), centimeter
(cm), milimetre (mm), mililitre (ml au Ml), litre (L au l) na siyo vinginevyo.
Kadhalika, Meneja Kabikiye amehimiza wajasiriamali
kuzingatia mambo kadhaa kwenye vifungashio vyao kama kuandika jina la
utambulisho wa bidhaa, kuandika jina na mahali anapofanyia biashara yake,
kuweka anuani ya posta, namba ya simu na barua pepe. Vilevile, mjasiriamali
anatakiwa kuainisha kiasi halisi cha bidhaa yake aliyofungasha mfano; (2 kg au
1 L) na ahakikishe anaacha nafasi moja kati ya namba na herufi mfano; 200g
(Sisahihi) 200 g (Sahihi).
Wakala wa Vipimo inaendelea kutoa wito kwa
Wafanyabiashara na Wajasiriamali wote kuzingatia matumizi sahihi ya Vipimo
katika uuzaji na ufungashaji wa bidhaa zao ili kuhakikisha hawajipunji na
hawawapunji wanunuzi wa bidhaa zao kwani kwa kufanya hivyo pande zote mbili
zitaendelea kunufaika na kukuza uchumi wa biashara zao na uchumi wanchi kwa
ujumla.