BODI YA USHAURI NA MENEJIMENTI YA WAKALA WA VIPIMO YAZUNGUMZA NA WATUMISHI WAKE.

Imewekwa:April 29, 2024

BODI YA USHAURI NA MENEJIMENTI YA WAKALA WA VIPIMO YAZUNGUMZA NA WATUMISHI WAKE.

Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Vipimo chini ya Mwenyekiti wake Profesa Elizabeth Alfred Mwakasangula imezungumza na watumishi wa taasisi hiyo leo tarehe 29,April 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF),Ilala Jijini Dar es salaam.

Katika kikao hicho profesa Mwakasangula amesema kuwa pamoja na mengine lengo la kikao hichi ni kutoa taarifa kuwa aliyekuwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala Bi.Stella Kahwa amestaafu rasmi Utumishi wa Umma hivyo amepongeza mamlaka zilizopo kumkaimisha ndugu Alban Kihulla kuwa Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo mpaka hapo itakapoamuliwa vinginevyo.`

Katika hatua nyingine Profesa Mwakasangula amewaasa watumishi wa Wakala kuheshimiana,kufanya kazi katika misingi ya haki na kuepuka rushwa na ukandamizaji,kujengea taswira njema ya Wakala kwa wateja pindi wanapo wahudumia na kutimiza malengo ambayo yamewekwa na taasisi, hii itapelekea taasisi kuheshimika na kujenga mahusiano mema na wateja.

“ Sasa hivi tunazidi kutanua wigo wa huduma zetu,tumeanza na Uhakiki wa Mita za Umeme,Dira za Maji na sasa tunatarajia kuanza uhakiki wa vifurushi (bando) katika matumizi ya simu na intaneti. Kwa hiyo tunatakiwa kuongeza juhudi zaidi katika utendaji kazi wetu ili kufikia malengo husika” Profesa Mwakasangula amesema.

Katika hatua nyingine kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo ndugu Alban Kihulla ameahidi kuwa daraja baina ya watumishi na Bodi ya Ushauri na kuahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi bila majungu kwani hii itasaidia kujenga uchumi na kuchochea ukuaji wa sekta mbalimbali.

Taasisi ya Wakala wa Vipimo imeendelea kutekeleza majukumu yake kikamilifu kwa kuzingatia sheria na kanuni mbalimbali za vipimo na za Utumishi wa Umma huku ikiendelea kutanua wigo wa huduma zake na kujenga misingi imara ya ukuaji wa kitaasisi.