Naibu Waziri Londo Aitaka Wakala wa Vipimo Kusimamia Sheria Kulinda Haki za Mlaji
Imewekwa:January 26, 2026
Naibu Waziri
wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, ameitaka Wakala wa Vipimo nchini kuongeza
uwajibikaji na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sheria za vipimo ili
kuwalinda walaji dhidi ya udanganyifu na kuhakikisha wanapata thamani halisi ya
fedha zao.
Londo amesema
usimamizi madhubuti wa vipimo ni msingi muhimu katika kujenga uchumi shindani,
himilivu na jumuishi, sambamba na kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo
ya 2025 na 2050.
Ameyasema
hayo wakati wa ziara ya kikazi katika Ofisi za Wakala wa Vipimo Mkoa wa Pwani,
ambapo amesisitiza kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara imejipanga kuhakikisha
kunakuwepo mazingira wezeshi ya biashara huku ikijenga imani kwa walaji katika
huduma na bidhaa wanazopata.
Naibu Waziri
ameongeza kuwa kutokuwepo kwa usimamizi sahihi wa vipimo kunawanyima walaji
haki zao za msingi na kudhoofisha ushindani wa haki katika biashara, jambo
linaloweza kuathiri ukuaji wa uchumi kwa ujumla.
Kwa upande
wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo amewasihi wananchi kushirikiana
na wakala huo kwa kutoa taarifa pindi wanapobaini kupatiwa huduma au vipimo
visivyo sahihi, akisema ushirikiano wa wananchi ni nyenzo muhimu katika
kudhibiti vitendo vya udanganyifu na kuimarisha haki katika biashara.
Wakala wa
Vipimo una jukumu la kuhakikisha vipimo vinavyotumika katika biashara vinafuata
viwango vilivyowekwa kisheria, hatua inayolenga kulinda maslahi ya walaji na
kukuza biashara yenye uadilifu nchini