ELIMU YA MATUMIZI SAHIHI YA VIPIMO YATOLEWA KWA WABUNGE

Imewekwa:May 21, 2024

Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Mhe. Omar S. Shaaban ameipongeza taasisi ya Wakala wa Vipimo (WMA) kwa namna inavyoendelea kusimamia usahihi wa vipimo katika sekta mbalimbali na kuhakikisha kunakuwa na haki baina ya pande mbili zinazofanya biashara.

Mhe. Omar ameyasema hayo alipotembelea banda la Wakala wa Vipimo mara baada ya kufungua maonesho ya wiki ya Viwanda na Biashara yanayofanyika katika viwanja vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yakiwa na lengo la kutoa elimu kwa waheshimiwa wabunge kuhusu majukumu na kazi zinazofanywa na taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara.

Kadharika, Mhe. Omar Shaaban ameipongeza taasisi ya Wakala wa Vipimo Bara (WMA) kwa kuendeleza mashirikiano na taasisi ya Wakala wa Vipimo Zanzibar (ZAWEMA) na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi hizo mara kwa mara ili kuhakikisha zinatimiza lengo kuu ambalo ni kumlinda mlaji kupitia matumizi sahihi ya vipimo.

Kupitia maonesho hayo yaliyoandaliwa na wizara ya viwanda na Biashara waheshimiwa wabunge mbali mbali wametembelea banda la wakala wa vipimo ambapo wamepata kufahamu kwa undani majukumu ya taasisi hiyo hususani katika maeneo ya uhakiki wa dira za maji na alama ambazo zinawekwa katika dira sahihi zilizohakikiwa, Uhakiki wa mita za umeme ambapo ni eneo jipya ambalo limeanza kufanyiwa kazi, pamoja na uhakiki wa pampu za kuuzia mafuta.

Vilevile, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo Bw. Alban Kihulla ametoa elimu kwa baadhi ya waheshimiwa wabunge kwenye eneo la ufungashaji wa mazao ya shamba ambapo amewaeleza kuwa kwa mujibu wa sheria ya Wakala wa Vipimo Sura Na. 340 mazao yoye ya shamba yanatakiwa kufungashwa kwa uzito usiozidi kilogramu mia moja (100 kg) na endapo gunia litafungashwa kwa uzito zaidi ya ule unaokubalika kisheria hatua zitachukuliwa dhidi ya msafirishaji na mmiliki wa mzigo.

Vilevile, katika maonesho yanayoendelea katika viwanja vya Bunge Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu Bw. Alban Kihulla amegawa zawadi ya picha yenye kaulimbiu ya maadhimisho ya siku ya vipimo duniani kwa wageni mbalimbali waliofika kupata elimu kwenye banda la wakala wa vipimo. Siku ya Vipimo Duniani imeadhimishwa katika mikoa yote ya kivipimo Mei 20, 2024 ikiwa na kaulimbiu “Tunapima leo kwa kesho endelevu” ambapo katika maadhimisho hayo wakala ilitoa mizani kwenye soko la Ilala Jijini Dar es Salaam ili kuhamasisha matumizi sahihi ya vipimo na kuacha kupima bidhaa kwa kutumia visado na makopo.

Wakala wa vipimo inaendelea kuwasihi wafanyabiashara na wamiliki wote wa vipimo kuhakikisha vipimo vyao vinakuwa sawa kila mara ili kutenda haki wakati wote bila kuwapunja watumiaji wa huduma katika maeneo yao.