ELIMU YA VIPIMO YATOLEWA KWA WATUMISHI WA NSSF MKOA WA TEMEKE

Imewekwa:June 24, 2024

Wakala wa Vipimo (WMA) imetoa elimu ya matumizi sahihi ya vipimo kwa watumishi wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mkoa wa Temeke.

Akitoa elimu hiyo katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano jengo la NSSF Ilala, Meneja wa sehemu ya viwango na uhakiki wa Wakala wa Vipimo Bw. Magesa Biyani amewajengea ufahamu watumishi hao kwa kuwaelimisha juu ya historia ya Wakala wa Vipimo, muundo wa utendaji kazi pamoja na majukumu ya Wakala ikiwa ni pamoja na kuwaelekeza namna dira za maji zinavyo hakikiwa, ukaguzi wa bidhaa zilizofungashwa unavyofanyika, uhakiki wa vituo vya mafuta pamoja na namna ya kutambua alama zinazowekwa katika mizani sahihi na iliyohakikiwa.

Sanjari na hayo, Bw. Magesa amejibu hoja na maswali mbalimbali yanayohusu vipimo yaliyowasilishwa kwake kutoka kwa watumishi wa NSSF, na amewapa ushauri wa kitaalamu juu ya matumizi sahihi ya vipimo katika Nyanja za biashara,afya, na mazingira.

“Maafisa Vipimo hawawezi kuwepo katika kila eneo kwenye mazingira yetu, ndio maana tunajikita katika kutoa elimu ya matumizi sahihi ya vipimo kwa wananchi na wadau ili kuwajengea ufahamu na umakini pale ambapo wanatoa huduma au kuhudumiwa katika namna mbalimbali. Kwa mfano ukiwa unakwenda kununua mbao buguruni, mwambie muuzaji kwamba ninaomba kipimo chako unachotumia (tape measure) ili nijiridhishe kama kipo sahihi, tunatakiwa kuwa makini katika mambo haya ya vipimo ili kuepuka hasara za matumizi mabaya ya vipimo” amesema Bw.Magesa.

Kwa upande wake Meneja wa NSSF mkoa wa Temeke Bw.Feruzi Mtika, ameishukuru Wakala wa Vipimo kwa kuwapa elimu na kuwajengea ufahamu juu masuala mbalimbali ya kivipimo.

Aidha, Bw.Feruzi ameahidi ushirikiano wa dhati baina ya NSSF na WMA katika Nyanja za vipimo na masuala mbalimbali ya kijamii ili kuimarisha uhusiano chanya kati ya taasisi hizo na kuleta maendeleo katika jamii.

WMA inaendelea kujikita katika utekelezaji wa majukumu yake sanjari na kutoa elimu ambayo huhusisha kuwafikia wananchi na wadau katika maeneo mbalimbali ili kuwajengea ufahamu juu ya matumizi sahihi ya vipimo ili kuleta usawa kati ya mtoa huduma na mteja, na kuepuka madhara yatokanayo na matumizi ya vipimo yasiyo sahihi.