KAMATI YA BUNGE VIWANDA, BIASHARA, KILIMO NA MIFUGO YAPATIWA ELIMU KUHUSU MATUMIZI SAHIHI YA VIPIMO

Imewekwa:November 21, 2023

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda Biashara, Kilimo na Mifugo imeielekeza Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia Wakala wa Vipimo nchini (WMA) kuwa na mpango mkakati endelevu wa utoaji elimu kuhusu matumizi sahihi ya Vipimo ili kuwajengea uelewa zaidi Wananchi kuhusu utambuzi wa Vipimo vilivyohakikiwa na kuwaeleza madhara ya kutumia Vipimo batili.

Wito huo umetolewa leo tarehe 21 Novemba 2023 Mkoani Kagera na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Viwanda ,Biashara ,Kilimo na Mifugo Mhe. Deodatus Mwanyika ( Mb) wakati wa Semina ya kujenga uelewa kuhusu kazi na majukumu ya Wakala wa Vipimo nchini (WMA).

Aidha, Mhe. Mwanyika ameelekeza Wizara kuwa na mkakati endelevu wa ukaguzi wa vipimo vinavyotumika katika maeneo mbalimbali nchini hususani kuanza mara moja na upimaji katika maeneo ya muda wa maongezi na taxi za mitandao, kwa kuwa maeneo hayo yanatumiwa sana na wananchi.

"Sisi kama kamati ya Bunge tunaosimamia na kuishauri Serikali tunnailekeza Wizara kuwa na zoezi endelevu la ukaguzi wa vipimo sahihi sambamba utoaji elimu kuhusu matumizi sahihi ya Vipimo hasa kwa wananchi wa chini ambao ndio walaji wa mwisho Ili kiasi cha fedha wanacholipa kiendane na kiasi cha bidhaa wanazonunua " Amesema Mwanyika.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb) akichangia katika Semina hiyo ameelekeza Wakala wa Vipimo nchini (WMA) kuzingatia mapenpekezo yote yaliyotolewa na kamati ya Bunge katika Semina hiyo na kutaka utekelezaji wake uanze mara moja Ili kuondoa matumizi ya vipimo batili.

"Kama Wizara Kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara tumepokea maelekezo ya Kamati na michango yote iliyotolewa kwenye Semina hii ,naelekeza wataalamu wetu kupitia WMA kuendelea kusimamia matumizi sahihi ya Vipimo na kutoa elimu na mafunzo mbalimbali kuhusu utumiaji wa Vipimo sahihi ili Wananchi wasipunjwe kupitia vipimo

Ameeleza Bw.Kigahe

Nae Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashill Abdallah ameishukuru Kamati ya Bunge kwa ushiriki wao katika Semina hiyo ambayo imelenga kutoa elimu kwa Kamati ya Bunge na kukagua miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Wizara iliyopo katika Mkoa wa Kagera.

Aidha, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo WMA Bi. Stella Kahwa ameishukuru kamati ya Bunge ya Viwanda Biashara, Kilimo na Mifugo kwa michango na maelekezo yao waliyotoa kuhusu usimamizi wa vipimo kwenye sekta mbalimbali ili kuhakikisha Wananchi wanapata bidhaa zilizo sahihi wakati wote na vipimo vinavyotumika vinakuwa sahihi wakati wote.