KAMATI YA KILIMO, BIASHARA NA UTALII YAIPONGEZA WAKALA WA VIPIMO KWA UTENDAJI KAZI WAKE
Imewekwa:March 07, 2023Kamati ya Kilimo, Biashara na Utalii Baraza la Uwakilishi Zanzibar imeipongeza taasisi ya Wakala wa Vipimo kwa utekelezaji mzuri wa majukumu yake katika kuhakikisha inawalinda watumiaji wa vipimo mbalimbali.
Akizunguamza
mara baada ya kufanya ziara ya kujifunza kwenye kituo cha uhakiki cha Wakala wa
Vipimo kilichopo Misugusugu Mkoa wa Pwani Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Yusuf
Hassan Iddi amesema, kupitia ziara hii wamejifunza mambo mengi kwakuwa na wao
upande wa Zanzibar wana taasisi kama hii ambayo inaitwa ZAWEMA japo kwa upande
wa Tanzania bara ilianza muda tangu mwaka 2002 hivyo kuna mengi ya kujifunza
ili kuweza kuishauri Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuiwezesha taasisi yake ya
Vipimo katika kusimamia usahihi wa vipimo kwenye maeneo mbalimbali.
Mhe.
Yusuf ameeleza kuwa taasisi hizi za vipimo ni muhimu sana kwa kuwa
zihahakikisha zinamlinda mtumiaji wa mwisho wa vipimo kupata vipimo sahihi ndiomana
hata kwenye sekta ya afya mgonjwa anapimwa kwanza uzito ili apate dozi inayoendana na uzito wake kwakuwa kinyume
na kufanya hivyo anaweza pata madhara. Kadhalika, kwenye usalama wakala wa
Vipimo inajukumu la kuhakiki tochi za maafisa wa usalama barabarani ili
kujiridhisha kama zinafanya kazi kwa usahihi lakini pia kwenye biashara taasisi
hizi za vipimo zinasaidia kuhakikisha Mwananchi anapata bidhaa kwa usahihi
kulingana na thamani ya fedha anayotoa bila kupunjwa.
Mhe.
Yusuf amesema kamati inaipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kwa kuiwezesha Wakala wa Vipimo kujenga kituo kikubwa na cha kisasa ambacho
kinafanya shughuli za upimaji wa matenki ya malori ya kusafirisha mafuta,
lakini pia, wamemeona mitambo ya kisasa ambayo inatumika kupima mita za maji na
umeme kabla hazijaenda kufungwa kwa wateja na upimaji huu utasaidia sana
kupunguza malalamiko kwa Wananchi wanaotumia huduma hizo ndio maana kama kamati
tutashauri ili na upande wa Zanzibar tuweze kupata kituo cha aina hii ili
kuwalinda watumiaji wa huduma hizo.
Kwa
upande wake Naibu Waziri Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Exaud
Kigahe (Mb) ameishukuru na kuipongeza kamati kwa kutembelea taasisi ya Wakala
wa Vipimo katika kituo chake cha Upimaji Misugusugu kwa ziara ya kujifunza kazi
zinazofanywa na taasisi hiyo ambapo wametembezwa na kushuhudia kazi mbalimbali
zinavyofanyika ikiwa ni pamoja na upimaji wa matenki ya malori ya kusafirisha
mafuta, upimaji wa mita za umeme pamoja na Dira za Maji.
Ameeleza
kuwa kupitia ziara hii anaamini watajifunza mambo mengi lakini pia ni fursa ya
kubadilishana mawazo ya namna ya kuboresha taasisi hizi na wamepokea ushauri
uliotolewa na Kamati hasa kwenye eneo la kuweka alama kwenye dip stick kutumika njia za kisasa zaidi
kuliko zinazotumika kwa sasa.
Akizungumza
na waandishi Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo Tanzania Bara Bi.
Stella Kahwa ameeleza kuwa ushirikiano baina ya Wakala wa Vipimo Zanzibar
(ZAWEMA) na Wakala wa Vipimo Tanzania Bara (WMA) umeanza muda kwa kushirikiana
kubadilishana uwezo wa kitaalamu na vitendea kazi ili kuhakikisha Wananchi
wanapata bidhaa zenye vipimo sahihi. Pia, taasisi hizi zinashirikiana hata
katika suala la kutoa elimu kwenye maonesho mbalimbali kama ya Mapinduzi na
elimu ya vipimo kwa Wafanyabiashara mbalimbali kama masonara wanaouza vito na
madini.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Vipimo Zanzibar (ZAWEMA) Bw.
Mohamed Simai ameishukuru Kamati ya Kilimo, Biashara na Utalii ya Baraza la
Uwakilishi Zanzibar kwa kutenga muda kuja kujifunza namna shughuli za vipimo
zinavyofanyika kwakuwa anaamini itawasaidia katika kuweza kuishauri Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kuiwezesha zaidi ZAWEMA ili iweze kutanua wigo wa
utekelezaji wa majukumu yake na kuhakikisha inawalinda Wananchi katika sekta
mbalimbali kwa kusimamia matumizi ya Vipimo sahihi.