KATIBU MKUU AKUTANA NA VIONGOZI WA WAKALA WA VIPIMO KUJADILI MAMBO YA KIUTENDAJI
Imewekwa:February 18, 2023
Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Hashiri Abdallah amewataka mameneja vipimo katika mikoa kuendelea kutoa elimu ya vipimo na kusimamia usahihi wa vipimo ili kuwalinda Wananchi. Hayo ameyasema Mkoani Morogoro tarehe 18 Februari, 2023 katika kikao kazi kilichowakutanisha mameneja vipimo nchini.
Aidha, amewasisitiza Kufanya kazi kwa bidii na kutengeneza mazingira ya kuwaelewesha wafanyabiashara umuhimu wa kuzingatia vipimo katika bidhaa wanazozalisha. Pia, amewataka kusimamia Sheria na utekelezaji wa sheria hizo kuwa wezeshi, ili mazingira ya ufanyaji biashara nchini yaendelee kuwa bora.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa idara ya maendeleo ya Biashara, Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara Bw. Sempeho Manongi amewataka mameneja hao kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia weledi kwa kuwa weledi ndio unapelekea kazi zifanyike kwa ufanisi.
Pia amewataka mameneja mikoa hao kuhakikisha mazingira ya kufanya biashara nchini yanayafanyika kwa haki kwa kuwa taasisi hiyo inashughulika bidhaa zinazozalishwa ndani na nje ya nchi.
Pia, aliitaka taasisi hiyo kufanya kazi kwa uwazi, ili kuepuka vitendo visivyofaa ambavyo vimekua vinaleta malalamiko kwa jamii.
Kwa upande wake Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu Bi. Stella Kahwa amemshukuru Katibu Mkuu kwa kutenga muda na kufanya kikoa na mameneja wote wa mikoa ya kivipimo Tanzania Bara na amehaidi kufanyia kazi maagizo yote yaliyotolewa kwa lengo la kusimamia usahihi wa vipimo katika sekta mbalimbali ili wananchi waweze kupata bidhaa zenye vipimo sahihi pasipo kupunjwa.
Kadhalika, amesema wakala itaendelea kufanya kaguzi mbalimbali za kushtukiza kwa lengo la kuendelea kuwalinda wananchi na wafanyabiashara wote nchini.