MKUU WA MKOA WA LINDI AHIMIZA MATUMIZI YA VIPIMO SAHIHI
Imewekwa:September 06, 2017
Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Godfrey W. Zambi amewataka Wakala wa Vipimo Kuongeza nguvu zaidi katika kusimamia matumizi sahihi ya vipimo katika maeneo mbalimbali, ili wakulima na Wananchi kwa ujumla waweze kunufaika na mazao wanayolima pindi waendapo kuyauza wakati wa msimu.
Mkuu wa Mkoa ameyasema hayo alipotembelea
banda la WMA, katika maonesho ya nane nane ambayo kitaifa yanafanyika katika
mkoa wa Lindi kwenye viwanja vya ngongo.
Pia amewataka Wakala wa Vipimo kushirikiana na maafisa waliopo katika
ofisi ya mkuu wa mkoa katika kuhakikisha wakulima hawapunjwi pindi waendapo
kuuza mazao yao. kwani baadhi ya
wafanyabiashara wasio waaminifu, huchezea
mizani yao kwa lengo la kuwapunja wakulima kwa lengo la kupata faida zaidi.
Vilevile Mhe. Godyfrey Zambi alielezwa na
maafisa wa vipimo namna kangomba inavyowapunja wakulima, kwa kuwa siyo kipimo
sahihi kinachopaswa kutumika kununulia mazao.
Hivyo Wakala wa Vipimo inawapa wakulima elimu ya matumizi sahihi ya mizani
iliyo hakikiwa. Pia wanaelekezwa namna
ya kutambua alama zinazowekwa kwenye vipimo vilivyohakikiwa na Wakala ambazo
ni stika maalum, pamoja na kugongwa nembo ya
Taifa na tarakimu mbili za mwisho za mwaka husika. Mfano kwa mwaka huu 2017, itasomeka
namba 17.
Akizungumza na mwandishi wetu baada ya ziara
ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Afisa Vipimo wa Lindi Bw. Nyagabona Mkanjabi amesema,
wamejipanga vizuri katika kusimamia matumizi ya vipimo sahihi na kuhakikisha
mizani zote zinazotumika katika vyama vya ushirika vya msingi zinakaguliwa
kabla ya misimu ya kuuza mazao kuanza. Pia watahakikisha kaguzi mbalimbali za
kustukiza zinafanyika kipindi cha msimu wa kuuza mazao unapofika.
Pia, amewakaribisha viongozi wa vyama vya
ushirika vya msingi pamoja na wananchi wote kutembelea banda la wakala wa
vipimo katika maonesho ya nanenane mkoa wa Lindi na kujionea Mizani mbalimbali
zinazopaswa kutumika katika ununuzi wa bidhaa mbali mbali na mazao ukiwemo
mzani wa digital wa tani 2 ambao unapima bidhaa/mazao na kutoa risiti hapo hapo
Kaimu Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Lindi
Bw. Andrew Mbwambo ametoa wito kwa Wakulima, wafanyabiashara na Wananchi wote
kutojihusisha na vitendo vya kuchezea vipimo kwani kwa sasa adhabu ni kubwa baada
ya Sheria ya Vipimo Sura namba 340 na Mapitio yake ya mwaka 2002 kufanyiwa
marekebisho mwaka 2016.