WAFANYABIASHARA WA MADINI WAHIMIZWA KUTUMIA VIPIMO SAHIHI GEITA

Imewekwa:September 26, 2025

Meneja wa Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Geita Bi. Eva Ikula amewataka wafanyabiashara wa madini mkoa wa Geita kuzingatia matumizi ya vipimo sahihi wakati wote ili kuhakikisha kunakuwa na usawa katika biashara hiyo bila upande wowote kupunjika.

Wito huo ameutoa tarehe 24 Septemba, 2025 alipozungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya kimataifa ya Teknolojia ya madini yanayofanyika Mkoa wa Geita katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan yenye kaulimbiu ya “Ukuaji wa Sekta ya madini ni matokeo ya matumizi ya teknolojia sahihi na uongozi bora, shiriki uchaguzi mkuu oktoba 2025”.

Bi. Eva Ikula ameeleza kuwa, Wakala wa Vipimo inamchango mkubwa katika sekta ya madini ambapo biashara hiyo haiwezi kufanyika bila kuwa na mizani iliyohakikiwa na inayotumika kwa usahihi ili kuhakikisha kunakuwa na usawa baina ya pande mbili zinazofanya biashara.

Kaharika, amesema Wakala wa Vipimo katika sekta ya madini inahakikisha mizani yote inayotumika kuuzia na kununulia vito na madini inahakikiwa na inapima madini kwa usahihi. Pia, Wakala inatoa ushauri wa kitaalamu juu ya mizani zinazopaswa kutumika kuuzia madini kwa kuwa siyo mizani yote inastahili kutumika kuuzia na kununulia madini.

“Mkoa wa geita kwa mwaka wa fedha 2025/2026 unatarajia kuhakiki mizani 197 inayotumika katika sekta ya madini ambapo mpaka sasa kwa robo ya kwanza jumla ya mizani 37 imehakikiwa na kukidhi vigezo kwa mujibu wa sharia ya Vipimo Sura 340 na inafaa kutumika katika uuzaji na ununuzi wa madini”. Amesema Bi. Eva.

Vilevile, Bi. Eva ameeleza kuwa Mkoa wa geita una jumla ya masoko kumi (10) ya kuuzia na kununulia dhahabu ambayo ni Geita mjini, Katoro, Chato, Lwamgasa, Nyarugusu, Mbogwe, Bukombe, Nyang’wale, Mgusu na Nyakagwe. Hivyo, Wakala wa Vipimo hufanya kaguzi za kushtukiza mara kwa mara kwa lengo la kijiridhisha kama vipimo vinatumika kwa usahihi na kwa mtumiaji yeyote ambaye hubainika kuchezea vipimo huchukuliwa hatua kwa mijibu wa Sheria ya Vipimo Sura 340.

Naye Afisa Mawasiliano Mwandamizi wa Wakala wa Vipimo Bw. Paulus Oluochi amewahimiza wananchi kufika kwenye banda la WMA kwa ajili ya kupata elimu ya vipimo na Ushauri wa kitaalamu kuhusu vipimo mbalimbali.

Pia, ameeleza endapo mtumiaji wa kipimo atapata changamoto yoyote aweze kuwasiliana na ofisi ya WMA iliyopo karibu ili aweze kupata msaada kwa haraka ambapo ofisi za WMA zinapatikana katika mikoa yote Tanzania Bara au atoe taarifa kwa namba ya bure ambayo ni 0800 110097.