MIZANI ZAIDI YA 225 IMEKAGULIWA KWA AJILI YA MSIMU WA UNUNUZI WA KAHAWA
Imewekwa:July 20, 2022
Wakala wa Vipimo (WMA) inaendelea na zoezi la ukaguzi wa mizani inayotarajiwa kutumika katika ununuzi wa zao la kahawa Mkoani Kagera. Ukaguzi huu hufanyika kila mwaka kabla ya kuanza kwa msimu wa ununuzi wa Mazao na mizani inayobainika kuwa sahihi uwekewa alama maalumu na Mkaguzi ambayo ni stika ya WMA na mizani yenye kasoro hukataliwa kutumika mpaka ifanyiwe marekebisho na fundi mizani mwenye lesseni kutoka Wakala wa Vipimo na mara baada ya matengenezo Mkaguzi hupita tena kukagua mzani kama upo sahihi unawekewa stika na kukubalika kutumika kununulia mazao.
Meneja wa WMA Kagera
Bi. Harrieth Lukindo amesema, Mpaka sasa ukaguzi umefanyika katika Wilaya za Missenyi
ambapo mizani 33 imekaguliwa, Muleba mizani 69 imekaguliwa, Bukoba mjini na
Vijijini mizani 68 imekaguliwa pamoja na Wilaya ya Karagwe na Kyerwa ambapo
zoezi bado linaendelea na mpaka sasa jumla ya mizani 60 imekaguliwa kwenye
vyama vya msingi.
Kadharika, Meneja
Harrieth amesema mara baada ya zoezi linaloendelea la kuhakiki mizani
kukamilika msimu unapoanza wa kununua kahawa Wakala wa Vipimo hupita na kufanya
ukaguzi wa kushtukiza kwenye vituo vya kununulia kahawa na kuhakiki kama mizani
inatumika kwa usahihi kama ilivyohakikiwa. Endapo chama chohote cha Msingi
kitajihusisha na uharibifu wa mizani hatua kali huchukuliwa dhidi yao kwa
mujibu wa Sheria ya Vipimo Sura Na. 340 na Mapitio yake ya mwaka 2002.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa zoezi hilo Bi. Stella Kahwa ambaye ni Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo alipokuwa Wilayani Kyerwa amesema kwamba msimu wa ununuzi wa Kahawa uanatarajiwa kufunguliwa kuanzia mapema mwezi Juni hivyo, ni lazima kuhakikisha vipimo vyote vitakavyotumika kwenye ununuzi wa Kahawa vinakaguliwa na mpaka sasa zoezi la ukaguzi linaendelea vizuri na limekamilika kwa asilimia 90 ambapo tunamalizia ukaguzi kwenye Wilaya za Karagwe na Kyerwa.