KAMATI YA BUNGE VIWANDA, BIASHARA NA MAZINGIRA YAIPONGEZA WAKALA WA VIPIMO
Imewekwa:November 18, 2022
KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE VIWANDA, BIASHARA NA MAZINGIRA YAIPONGEZA WAKALA WA VIPIMO KWA KUJENGA KITUO CHA UHAKIKI WA VIPIMO
Kituo cha Wakala wa
Vipimo (WMA), Misugusuru Mkoa wa Pwani kimekuwa cha mfano na nchi za Afrika
Mashariki zimekuwa zikija kujifunza ubora wa kazi zinazofanywa kwenye kituo
hicho.
Kituo hicho kimekuwa
kikitumika kuhakiki ujazo wa mafuta kwenye malori, kuhakiki mita za maji na
umeme kilijengwa kwa gharama ya Shillingi bilioni saba.
Hayo yalisemwa jana na
Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe (Mb), wakati
wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira,
iliyotembelea kituo hicho.
Naibu Waziri alisema
kituo hicho ni kipya na kimekuwa mfano bora kutokana na kazi zinazofanywa kiasi
cha kuwavutia watu wa nchi jirani kuja mara kwa mara kujifunza kuhusu vipimo.
“Kituo hiki kinafanya
kazi nzuri na kitaendelea kuwa mfano hivyo tunaamini mheshimiwa Rais ataendelea
kutupa fedha tujenge vituo kama hivi kwa kanda kama ambavyo kamati ya Bunge
imeshauri,” alisema Naibu Waziri Kigahe.
Kaimu Ofisa Mtendaji
Mkuu wa (WMA), Bi. Stella Kahwa, alisema wabunge wameona hatua kubwa
iliyofikiwa lakini wameshauri kuwe na maabara inayotembea ili kwenda kukagua
mita za maji na umeme kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Mwenyekiti wa Kamati
Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, Mhe. David Kihenzile alisema
wameona namna mita za maji zinavyohakikiwa na zile za umeme kuhakikisha
mwananchi anapewa mita ya maji au umeme yenye ubora ili alipe kile tu
anachotumia.
Alipongeza utaratibu
huo ambao alisema unamwezesha mwananchi kulipia kile ambacho anatumia na
alishauri WMA iendelee kukagua mita hizo kuhakikisha zinakuwa na ubora wa hali
ya juu ili kulinda maslahi ya mwananchi.
“Changamoto ambayo
tumeiona ni kwamba hivi mtu anayetengeneza mita za maji Katavi au Shinyanga
atazisomba zote aje zipimwe hapa Kibaha. Kwa hiyo tumewashauri wakala watazame
haya mbeleni ikiwezekana vituo kama hivi vijengwe kwenye kanda lakini kwa kweli
wanafanyakazi nzuri sana,” alisema