ELIMU KWA UMMA
Imewekwa:May 19, 2021
WAKALA WA VIPIMO YAENDELEA KUTOA ELIMU YA VIPIMO KATIKA MIKOA YA KUSINI
Wakala wa Vipimo (WMA) imeendelea kutoa elimu ya
matumizi sahihi ya Vipimo kwa Wafanyabiashara, Wajasiriamali na Viongozi wa
vyama vya msingi vya Ushirika (AMCOS) katika Mkoa wa Lindi. Elimu hiyo ni
muendelezo wa kuhakikisha wananchi na wafanyabiashara wanafahamu majukumu ya
taasisi hiyo na kufanya kazi zao kwa kuzingatia kanuni na Sheria ambazo
zinasisitiza matumizi sahihi ya vipimo katika utoaji wa huduma mbalimbali na si
matumizi ya vipimo batili kama kangomba.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa elimu kwa
umma Katibu Tawala Mkoa wa Lindi Bi. Rehema Madenge ambaye alimuwakilisha Mkuu
wa Mkoa amesema elimu hiyo ya Vipimo imefika kwa wakati muafaka ambapo msimu wa
ununuzi wa mazao unakaribia kuanza na alitumia wasaha huo kuwasihi viongozi wa
vyama vya Msingi vya Ushirika kuhakikisha kuwa mizani zote zitakazotumiwa
katika ununuzi wa mazao zihakikiwe na kuwekewa alama maalumu za Wakala wa
Vipimo kama vile stika pamoja na Lakili (seal).
Bi. Rehema amewaeleza wafanyabiashara na viongozi wa
vyama vya msingi kuwa wizi wa aina yeyote ni kosa la jinai hivyo hata kuibia
wananchi na wakulima kwa kuchezea vipimo ni kosa la jinai na yeyote atakaye
kamatwa kujihusisha na vitendo vya uchezeaji wa vipimo atakamatwa na
kuchukuliwa hatua stahiki. “Nawasihi sana wanunuzi wa mazao kuacha kutumia
vipimo batili kwakuwa kufanya ivyo ni kuwanyonya wakulima ndiomaana
wafanyabiashara wanaendelea kwa kasi huku wakulima wanabaki katika hali duni ya
kiuchumi itoshe kusema vitendo hivyo havikubaliki imefika wakati mkulima
inabidi apate tija kunufaika na kile anachokizalisha kwa kuuza mazao kwa
kutumia vipimo sahihi (mzani)” Katibu Tawala Mkoa wa Lindi alieleza.
Kadhalika, Bi. Rehema Madenge ameipongeza Wakala wa
Vipimo kwa kuendelea kupanua wigo wa kazi za vipimo katika maeneo mapya ambapo
kwa sasa taasisi hiyo inafanya uhakiki wa dira za maji pamoja na mita za umeme,
kwa kuzingatia hilo Bi. Rehema ameagiza Mamlaka ya maji Mkoa wa Lindi Luwasa
kuhakikisha wateja wote wapya na wazamani wanafungiwa mita za maji
zilizohakikiwa na Wakala wa Vipimo na kuwekewa alama maalumu ambayo ni lakiri
(seal).
Akizungumza
na mwandishi wetu Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Lindi ndugu, Andrew
Mbwambo amesema kuwa Wakala wa Vipimo inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa
Sheria ya Vipimo Sura Na. 340 na mapitio yake mbalimbali hivyo, mizani za
wafanyabiashara wadogo na zile zitumikazo katika vyama vya msingi vya ushiriki
kwa kawaida hufanyiwa uhakiki mara moja kwa mwaka na mara baada ya kumaliza
kaguzi mbalimbali za kushtukiza hufanyika katika maeneo hayo ili kujiridhisha
kama vipimo vinatumika kwa usahihi kama vilivyohakikiwa awali.
Meneja
Mbwambo amewaonya wafanyabiashara na
viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika kujiepusha na vitendo vya uchezeaji wa vipimo
kwa lengo la kutaka kujipatia faida zaidi kwani kufanya hivyo ni kinyume cha
Sheria ya Vipimo Sura na. 340 na mapitio yake mbalimbali ambayo inaeleza adhabu
kwa mtu atakaye kutwa amechezea vipimo ni faini isiyopungua shilingi laki moja
(100,000/=) na isiyozidi millioni ishirini (20,000,000/=) inategemea na ukubwa
wa makosa.
Vilevile,
wakati wa mafunzo wafanyabiashara na Viongozi wa AMCOS walielezwa madhara
mbalimbali yatokanayo na matumizi yasiyo sahihi ya vipimo ambayo ni pamoja na
kukiuka Sheria ya Vipimo ambayo inaweza kusababisha mfanyabiashara au Chama cha
Ushirika kuadhibiwa kwa kulipa faini au kupata adhabu ya kifungo mahakamani na
mali yake kutaifishwa. Pia, kumuibia mteja kwa kumpunja ni moja wapo ya wizi na
nikinyume na maandiko ya vitabu vitakatifu, lakini vilevile biashara zinaweza
kufa ama kufirisika kwa kuzidisha bidhaa kwa wateja pasipo kutumia vipimo
vilivyo sahihi katika biashara.
Akizungumza
na mwandishi wetu baada ya kupata mafunzo hayo Bw. Abubakari Mbalala ambaye ni kiongozi
wa Mnacho AMCOS amewapongeza sana Wakala wa Vipimo kwa kuwapatia elimu kuhusu
matumizi ya vipimo sahihi kwani na wao kama viongozi wataenda kulisimamia na
kuhakikisha katika msimu huu unaotarajia kuanza hivi karibuni mizani zote
zitakazotumika zitakuwa zimehakikiwa na zitatumika kwa usahihi ili kuepuka
kuwapunja wakulima wa zao la korosho na ufuta. Pia, wameiomba wakala wa vipimo
kuendelea kutoa semina za vipimo mpaka wilayani ili kuwafikia watu wengi zaidi
ili waweze kupata kuelewa namna ya kutumia vipimo sahihi.
Meneja
wa Wakala wa Vipimo Lindi Bw. Andrew Mbwambo ametoa wito kwa watumiaji wote wa
vipimo kuzingatia matumizi sahihi ya vipimo na endapo wataitaji ushauri wa
kitaalamu wasisite kutembelea ofisi za wakala wa vipimo zilizopo Mtaa wa Elieti
au kupiga namba ya simu ya bure 0800 110097.