Elimu kwa Umma pamoja na uhakiki wa mizani Wilayani Masasi Mkoani Mtwara

Imewekwa:August 11, 2017

JUMLA YA MIZANI 153 YAHAKIKIWA KATIKA VYAMA VYA WAKULIMA WILAYANI MASASI NDANI YA SIKU SITA

Wakala wa Vipimo (WMA) wa Vipimo Tanzania imeendelea na zoezi la utoaji wa elimu pamoja na uhakiki wa mizani kwenye vyama mbalimbali vya wakulima ( AMCOS) Wilayani Masasi Mkoani Mtwara ikiwa ni maandalizi ya msimu wa korosho pamoja na mazao mengine kama vile choroko, mbaazi pamoja na ufuta.

Kaimu Meneja Sehemu ya Elimu, Habari na Mawasiliano Bi. Irene John alisema kwa muda wa siku sita tayari wametembelea vyama vya msingi 46 na kukagua jumla ya mizani 153, kati ya hizo mizani iliyokutwa sahihi ni 104 na jumla ya mizani 52 ilikutwa na mapungufu hivyo haitaruhusiwa kwa biashara mpaka itengenezwe na mafundi na kuhakikiwa kwa upya na Wakala wa Vipimo ili iweze kuruhusiwa kwa ajili ya kutumika kibiashara.

Bi. John alitaja baadhi ya majina ya vyama hivyo kuwa ni Temeke, Tuaminiane, Mshikamano, Mpindimbi, Chamali, Chigugu, Mkaramani, Mumbaka, Masunge, Chamaka pamoja na Nami. “ kila kituo tunatoa elimu inayohusu matumzi sahihi ya mizani, namna ya kutunza mizani pamoja na kuhakiki mizani inayotumiwa na vyama vya wakulima ( AMCOS) ili vyama hivyo vitakapotoa zabuni kwa mafundi mizani iwe ni ile tu iliyopimwa na kuonekana na hitilafu na siyo kupewa zabuni ya mizani yote yaani iliyosahihi na isiyosahii, na hii itampunguzia mkulima gharama “ alisema bi. Irene.

Kaimu Meneja Bi. John aliwasihi baadhi ya wakulima wanaolalamikiwa kuweka mawe, kokoto pamoja na mchanga kwenye Korosho, Ufuta, Mbaazi pamoja na Choroko kwa ajili ya kuongeza uzito waache tabia hiyo mara moja sababu Sheria ya vipimo ipo na inafanyakazi kwa pande zote mbili muuzaji na mnunuzi wote kwa pamoja hawatakiwi kufanya udanganyifu wowote katika biashara.

Irene alisema Sheria ya Vipimo Sura 340 inawataka Wakala wa Vipimo kuhakiki na kupiga chapa vipimo vyote vinavyotumika katika biashara pia Wakala wa Vipimo imeongeza na stiker kwa kipimo kitakachokuwa tayari kimehakikiwa ili iwe rahisi kwa wakulima kuona na kutambua mizani iliyokaguliwa na kuruhusiwa kwa biashara kwa mwaka husika.

Alisisitiza kuwa kwa wale watakaobainika kuchezea mizani kwa ajili ya kuwaibia wakulima adhabu ni kuanzia laki moja hadi milioni ishirini endapo mkosaji atakubali kosa, endapo kesi itafika mahakamani na mlalamikiwa akakutwa kweli alikosa kulingana na ushahidi utakaokuwa umetolewa mshitakiwa atatozwa faini kuanzia laki tatu hadi milioni hamsini au kifungo cha miaka mitatu au vyote kwa pamoja. Lengo kuu ni kumlinda mlaji ili apate faida na thamani ya kile alichozalisha na siyo kupunjwa na wafanyabiashara wajanjawajanja.

Tunaimani Tanzania ya viwanda itafanikiwa tena sana endapo Mkulima, Mfanyabiashara watazingatia matumzi ya vipimo sahihi kuanzia maandalizi ya shamba, upandaji wa mazao, utumiaji wa pembejeo, uuzaji, usafarishaji, upokea wa mazao, ufungashaji hadi utumiaji wa mazao yenyewe , hivyo vyote vikizingatia matumizi ya vipimo sahihi viwanda vingi vitaweza kupata malighafi za kutosha sababu mkulima na mfanyabiashara kila mtu atakuwa na imani na mwenzake kupitia matumizi ya vipimo sahihi. Msema kweli na mleta haki katika biashara ni kipimo sahihi kilichohakikiwa na Wakala wa Vipimo wala siyo vinginevyo.

Zoezi hili bado linaendelea na baada ya kukamilisha Wilaya ya Masasi wanatarajia kuhamia Wilaya ya Nanyumbu kwa ajili ya utoaji wa elimu pamoja na uhakiki mizani itakayotumika kununulia Korosho kwa msimu wa mwaka 2017/2018.

Zoezi hili pia linaendelea Mkoani Lindi ambapo jumla ya Mizani 89 imekaguliwa kati ya hizo 46 ilikutwa iko sahihi na 43 ilikutwa na hitilafu mbalimbali, hivyo hiyo yenye mapungufu itafanyiwa matengenezo na mafundi ili ihakikiwe upya na Wakala wa Vipimo kwa ajili ya kuruhusiwa kama ikiwa sahihi au kutoruhusiwa endapo itaendelea kuonesha mapungufu mara baada ya matengenezo.