Elimu kwa Umma kwenye viwanja vya Maisara Zanzibar
Imewekwa:December 09, 2021
WAKALA WA VIPIMO TANZANIA BARA NA ZANZIBAR WALISHIRIKIANA KUTOA ELIMU KUHUSU MATUMIZI SAHIHI YA VIPIMO KWENYE MAONESHO YA 6 YA BIDHAA ZA VIWANDA.
Wakaazi
wa Zanzibar wamehimizwa kujitokeza kwa wingi kwenye Viwanja vya Maisara kwa
lengo la kupata elimu kuhusu matumizi sahihi ya Vipimo. Elimu ya Vipimo
inatolewa kwa ushirikiano wa taasisi mbili ambazo ni Wakala wa Vipimo Tanzania
Bara (WMA) na Wakala wa Vipimo Zanzibar (ZAWEMA).
Akizungumza
na mwandishi wetu Mkurugenzi wa Vipimo Zanzibar Bw. Mohammed Mwalim Simai amesema,
kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo Wakala wa Vipimo ndio taasisi pekee inayosimamia matumizi sahihi ya vipimo kwa
kuhakikisha kuwa vipimo vinavyotumika
katika biashara viko sahihi, ili kuwalinda walaji na watumiaji wa vipimo.
Kuzingatia matumizi sahihi ya vipimo kutaepusha madhara yatokanayo na vipimo
batili.
Wananchi
wakitembelea banda la Wakala wa Vipimo watapata kufahamu majukumu
yanayotekelezwa na taasisisi hiyo ikiwa ni pamoja na kufanya uhakiki wa vipimo
mbalimbali kama vile mizani inayotumika kwenye maduka ya kuuzia nyama na bidhaa
mbalimbali za majumbani, kutoa ushauri wa kitaalamu kwa watumiaji wa vipimo,
kudhibiti vipimo vinavyotumika na vivavyopaswa kutumika katika biashara.
Alisema Mkurugenzi Mohammed.
Akizungumza
na mwandishi wetu meneja wa Wakala wa Vipimo Kitengo cha Bandari Tanzania Bara
Bw. Peter Chuwa ameeleza, Wakala wa Vipimo kadhalika inasimamia usahihi wa kiasi cha
mafuta yanayoingia nchini kwa njia ya Meli ili kuhakikisha kiasi cha
mafuta kilichoagizwa na Serikali kinapokelewa kikiwa sahihi. Lakini pia,
uhakiki unafanyika katika flow meters
zinazotumika kupokelea mafuta ambapo uhakiki wake hufanyika kila baada ya miezi
kumi na mbili ili kujiridhisha usahihi wake. Vilevile, Wakala wa Vipimo
inahakiki matenki makubwa ya yanayotumika kuhifadhia mafuta (fixed storage tanks), uhakiki wa matenki
ya malori yanayotumika kusafirisha mafuta ambayo pia huhakikiwa mara moja kila
baada ya miezi kumi na mbili (12).
Meneja
chuwa kadhalika amesema, uhakiki hufanyika kwenye vituo vya kujazia mafuta kwa
kuhakiki pampu zinazotumika kujaza mafuta kwenye vituo vyote vya kuuzia mafuta,
pampu zikihakikiwa na kuwa sahihi huwekewa alama maalumu ya utambuzi ambayo ni
stika maalumu inayoonesha pampu hiyo kuwa imehakikiwa. Pia, uhakiki hufanyika
kwenye visima vya kuhifadhia mafuta ardhini (Underground tanks), matenki hayo uhakikiwa mara moja kila baada ya
miaka mitano (5).
Wakala
wa vipimo kadhalika, imepata wasaa wa kuwatembelea wajasiriamali mbalimbali
kwenye maonesho ya bidhaa za Tanzania na kuangalia bidhaa zinazozalishwa na
kufungaswa na wajasiriamali wandani. Baadhi ya wazalishaji wa bidhaa hizo wamefungasha
vizuri bidhaa zao na kuweka alama za vipimo kwa usahihi, wajasiriamali ambao wamefungasha
bidhaa bila kuzingatia matumizi sahihi ya vipimo, wamepatiwa elimu ya namna
bora ya kufungasha bidhaa na namna
sahihi za kuandika alama za vipimo kwenye bidhaa zao kwa lengo la kuongeza
thamani ya bidhaa wanazozalisha ili ziweze kushindana kitaifa na kimataifa.
Mkurugenzi
wa Vipimo Zanzibar Bw. Mohammed Simai ameeleza kuwa, Wakala wa Vipimo
itaendelea kutoa huduma bora kwa kuwalinda watumiaji wa vipimo kwa kuingia
katika maeneo mapya ya utendaji kazi, kama inavyofanyika sasa upande wa Wakala
wa Vipimo Tanzania Bara, ambao wameanza kufanya uhakiki wa mita za maji zote
zinazoingizwa katika matumizi na uhakiki wa mita za umeme. Uhakiki wa mita za
umeme na maji upande wa Tanzania bara unafanyika katika kituo cha uhakiki
kilichopo kibaha Misugusugu mkoa wa Pwani, Kilimanjaro na vituo vya uhakiki
vilivyojengwa katika baadhi ya mikoa ya Wakala wa Vipimo bara. Hivyo, kwa hatua
waliyoipiga Wakala wa VipimoTanzania bara na upande wa Zanzibar tunajijengea uwezo
ili tuweze kuingia kwenye usimamizi wa vipimo kwenye maeneo hayo mapya ili
wananchi wapate huduma sahihi kulingana na thamani ya fedha yao.
Mkurugenzi
Mohammed amemalizia kwa kueleza kuwa endapo vipimo vitasimamiwa kwa usahihi itasaidia
Serikali kukusanya kodi kwa usahihi kutoka katika bidhaa mbalimbali zinazozalishwa
nchini na bidhaa zinazoingizwa kutoka nje ya nchi. Kadhalika vipimo visipo simamiwa kwa usahihi
itasababisha wananchi kupunjwa na kupata huduma au bidhaa ambazo haziendani na
thamani ya fedha wanayotumia.
Mkurugenzi
Mohammed ametoa wito kwa Wananchi na wafanyabiashara wote wa Tanzania bara na
Zanzibar kuhakikisha wanatumia vipimo sahihi na endapo watakutana na changamoto
yoyote inayohusu vipimo wafike kwenye ofisi za Wakala wa Vipimo kwa ajili ya kupata
msaada wa kitaalamu. Wamiliki wa vipimo
wameonywa kutochezea vipimo kwa lengo la kuwaibia wananchi, kwani kufanya hivyo
ni kosa kisheria na hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wote watakaobainika
kufanya vitendo hivyo ambavyo vinakatazwa hata kwenye maandiko matakatifu.