SETI 25 ZA VIPIMO VYA MAWESE ZAGAWIWA KWENYE MAADHIMISHO YA SIKU YA VIPIMO DUNIANI MKOANI KIGOMA

Imewekwa:May 21, 2023

Wakala wa Vipimo imeadhimisha siku ya Vipimo Duniani Mkoa wa Kigoma kwa kugawa jumla ya seti za vipimo 25 zenye ujazo wa lita 5, lita 10 na lita 20 kwa lengo la kuhimiza matumizi ya vipimo sahihi wakati wa uuzaji na ununuzi wa mawese na kuachana na matumizi ya vipimo batili maarufu kama bidoo ambayo huwanyonya na kuwapunja wakulima wakati wa mauzo.

Maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani huadhimishwa kila mwaka ifikapo mwezi Mei tarehe 20 na Kaulimbiu ya maadhimisho haya kwa mwaka 2023 ni Vipimo katika kuwezesha mfumo wa usambazaji wa chakula duniani.

Jumla ya vikundi vya Wakulima ishirini na nne (24) vimepatiwa vipimo hivyo ambapo Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo Bi. Stella Kahwa ameziomba halmashauri za Mkoa wa Kigoma kuona haja ya kutenga fedha na kununua vipimo vingine ili kuwasaidia wakulima kuuza mawese kwa kutumia vipimo sahihi na kutekeleza kampeni ya kutokomeza matumizi ya vipimo batili inayosema “bidoo sasa basi”.

Bi. Stella ameeleza kuwa jukumu la kusimamia haki katika biashara ambalo lipo katika Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara linatekelezwa na Wakala wa Vipimo ikiwa ni taasisi mwanachama wa Shirika la Vipimo Duniani (OIML) Shirika ambalo hutoa miongozo mbalimbali kuhusiana na Vipimo baada ya kufanya tafiti za kisayansi. Ameeleza kuwa mwaka 1875 nchi mbalimbali zilikutana nchini Ufaransa na kwa pamoja waliamuwa kuweka mlingano ili kipimo kitachotumika katika nchi moja kiwe sawa sawa na kipimo kitachotumika katika nchi nyingine ndio maana hata vipimo tulivyoleta na kukabidhi kwenye maadhimisho haya vina usahihi wa hali ya juu na vimewekewa alama maalumu uhakiki ambayo ni muhuri wa bibi na bwana.

Kwa upande wake Mgeni Rasmi Mhe. Kanali Isack Mwakisu Mkuu wa Wilaya ya Kasulu ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Geita Kamishna Jenerali Mstaafu wa Jeshi la Zima Moto na Uokozi Mhe. Thobias Andengenye ameupongeza uongozi wa Wakala wa Vipimo kwa kuchagua kufanya maadhimisho Kitaifa kwenye Mkoa wa Kigoma na kwa kuona umuhimu wa kutengeneza vipimo seti 25 ambavyo vimegawiwa kwenye vikundi mbalimbali vya Wakulima kwa ajili ya kuhimiza matumizi sahihi ya Vipimo na kuachana na Vipimo batili maarufu kama bidoo.

Kanali Mwakisu ameeleza kuwa vipimo vinatumika kwa namna mbalimbali kwenye maisha yetu ya kila siku na katika shughuli za kilimo vipimo hutumika kuanzia uandaaji wa shamba, kupanda mbegu, umwagiliaji, uwekaji wa mbolea shambani hadi wakati wa uvunaji na usambazaji wa mazao. Ameeleza kuwa vipimo ni nyenzo muhimu ambayo hutumika wakati wa kuuza hata wakati wa kusafirisha mazao kutoka sehemu moja hadi nyingine hivyo, wakulima wote wanapaswa kuzingatia matumizi sahihi ya vipimo kwenye mfumo mzima wa uzalishaji na usambazaji wa chakula.

Kwa upande wake Bi. Amina Mohamed ambaye ni mkulima na muuzaji wa mawese Wilaya ya Buhigwe amesema vipimo walivyopatiwa vitawasaidia kuuza mawese kwa kutumia vipimo sahihi siyo tena kwa njia ya ndoo kwani wanunuzi walikuwa wanawapunja kwa kutaka kujaziwa mawese kwenye ndoo kwa ujazo wa hadi kufikia kumwagika kitendo ambacho kilikuwa kinawasababishia hasara kubwa na kumnufaisha mnunuzi.