WAKALA WA VIPIMO TANZANIA NA ZAMBIA KUSHIRIKIANA KUSIMAMIA MATUMIZI SAHIHI YA VIPIMO
Imewekwa:January 26, 2026
Lusaka, Zambia
Taasisi za Wakala wa Vipimo kutoka nchini Tanzania
(WMA) na Zambia (ZMA)
zimesaini rasmi Mkataba wa kushirikiana katika usimamizi wa matumizi sahihi ya vipimo.
Mkataba huo ni wa muda wa miaka mitatu (3) ambapo utekelezaji wake umeanza mara
tu baada ya kusainiwa.
Kusainiwa
kwa Mkataba huo ni sehemu ya maono ya Viongozi wakuu wa nchi za Tanzania na
Zambia ambapo katika siku 100 za uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tangu
kuapishwa kwake amefanikisha utiaji saini baina ya taasisi ya WMA na ZMA kwa
lengo la kuweka mazingira rafiki ya ufanyaji Biashara hususani kwenye sekta ya
Vipimo.
Kusainiwa
kwa Mkataba huo pia ni matokeo ya ziara ya kikazi ambayo ilifanywa na Wakala wa
Vipimo Zambia (ZMA) kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya mafuta nchini humo
ambapo wakati wa ziara hiyo walishuhudia namna Serikali ya Tanzania imeiwezesha
Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia taasisi yake ya WMA kununua vifaa vya
kisasa na ujenzi wa kituo kikubwa Afrika Mashariki na Kati cha kuhakiki Vipimo katika
eneo la Kibaha, Mkoa wa Pwani.
Hafla
ya utiaji saini imefanyika Jijini Lusaka, Zambia tarehe 11 Disemba, 2025 na
kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali na
wataalamu kutoka nchi zote mbili, kwa upande wa Zambia wakiongozwa na Waziri wa
Viwanda na Biashara Mhe. Chipoka Mulenga (Mb) na upande wa Tanzania ukuongozwa
na Mhe. Lt Gen Mathew Edward Mkingule, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
nchini Zambia akimuwakilisha Dkt. Hashil T. Abdallah, Katibu Mkuu Wizara ya
Viwanda na Biashara.
Chini
ya Makubaliano hayo, mataifa hayo mawili yatatambua matokeo ya vipimo, vyeti
vya uthibitisho, idhini za aina (type approvals), na uthibitishaji wa kisheria
kutoka upande mmoja hadi mwingine. Mpango huu unatarajiwa kupunguza kwa kiasi
kikubwa vikwazo vya kitaalamu katika biashara, kuboresha ulinganifu wa
udhibiti, na kuongeza usahihi wa Vipimo katika biashara kwa lengo la kuwalinda
walaji kutoka pande zote.
Akizungumza
wakati wa ufunguaji wa hafla hiyo Waziri wa Viwanda na Biashara wa Jamhuri ya Zambia
Mhe. Chipoka Mulenga (Mb), ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa kuridhia taasisi ya Vipimo Tanzania na Zambia kushirikiana katika
usimamizi wa Vipimo kwakuwa kumekuwa na sintofahamu kwa muda mrefu kwenye
usimamizi wa vipimo baina ya Tanzania na Zambia, ambapo awali kila taasisi ya
vipimo haikuwa ikitambua upimaji unaofanywa na mwingine na hivyo kupelekea ucheleweshwaji wa huduma
kwa wafanyabiashara na watoa huduma ya uchukuzi katika Ushoroba wa Uchukuzi wa
Dar es Salaam na katika vituo vya kutolea huduma ya pamoja mipakani ikiwemo
Kituo cha Tunduma/ Nakonde.
“Makubaliano
haya yataondoa vikwazo katika biashara
na kuchelewa kwa bidhaa katika mipaka yetu kwani kwa sasa bidhaa
zitakazokaguliwa na WMA nchini Tanzania zitakubalika na kutambuliwa kutumika
nchini Zambia na kadhalika, bidhaa zitakazo kaguliwa na ZMA nchini Zambia
zitakubalika nchini Tanzania bila kikwazo.” alisema Waziri Chipoka Mulenga wakati
wa hotuba yake.
Makubaliano
hayo pia yanabainisha ushirikiano katika mafunzo ya pamoja, utafiti na
maendeleo, kubadilishana utaalamu wa kiufundi, na ushiriki hai katika majukwaa
ya kikanda na kimataifa ya vipimo kama OIML, SADCMEL, na AFRIMETS. Ushirikiano
huu utawezesha taasisi zote mbili kuendelea kuoanisha mbinu bora na teknolojia
za kisasa za vipimo zitakazotumika kwa manufaa ya pande zote mbili na kuigwa
kikanda.
Naye
Balozi wa Tanzania nchini Zambia Mhe. Lt Gen Mathew Mkingule amesema
ushirikiano baina ya taasisi ya Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) na Zambia (ZMA)
utasaidia kuondoa malalamiko hasa kwa upande wa wasafirishaji wa bidhaa za
mafuta na wamiliki wa vituo vya mafuta ambao kwa muda mrefu wamekuwa kwenye
sintofahamu na sasa biashara hiyo inaenda kuimarika zaidi kwakuwa vipimo
vitakavyo tumiwa na nchi hizi mbili vitakubalika na pande zote.
Akizungumza
katika hafla hiyo, Prof. Eliza Mwakasangula Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa
Vipimo (WMA) amesema Bodi itahakikisha inasimamia utekelezaji wa makubaliano
yaliyosainiwa kwa kuhakikisha Mkataba huu unatekelezwa kwa ufanisi, usimamizi
na mwelekeo wa kisera unatolewa ipasavyo, mfumo wa ufuatiliaji na tathmini
unafanya kazi, uwezo wa kitaasisi, miundombinu na ujuzi vinaimarishwa, pamoja
na kuhakikisha ushirikiano unabaki hai kupitia mapitio ya pamoja ya kila mwaka.
“Bodi
ya Ushauri ya Wizara itaendelea kuunga mkono Menejimenti kuhakikisha kwamba
ushirikiano huu unatoa matokeo yenye tija kwa mataifa yote mawili kwa lengo la
kuwalinda walaji.” Alisema Prof. Eliza Mwakasangula.
Katika
tukio hilo, sekta binafsi ya Jamhuri ya Zambia iliwakilishwa na Chama cha
Wasafirishaji wa Petroli cha Zambia Bw. Benson Tembo ambaye aliipongeza
Serikali ya Tanzania na Zambia kwa mafanikio yaliyofikiwa kupitia Taasisi hizo
za vipimo. Alibainisha kuwa taratibu zilizorahisishwa zitasaidia kuchagiza
ukuaji wa biashara ndogo na za kati na hivyo wadau wengi watavutiwa kufanya
biashara rasmi, jambo ambalo litasaidia katika kufikia malengo ya biashara za
uwili na kikanda mathalani SADC na Eneo Huru la Biashara Barani Afrika
(AfCFTA).
Wakala wa Vipimo (WMA) itaendelea kusimamia usahihi wa vipimo wakati wote kwa lengo la kuwalinda walaji kwa kuzingatia miongozo mbalimbali inayotolewa Kikanda na Kimataifa.