Ukaguzi wa Mizani Mtwara

Imewekwa:April 08, 2019

WAKALA WA VIPIMO (WMA) YAENDELEZA KAGUZI ZA KUSHTUKIZA KATIKA VITUO VYA KUNUNULIA KOROSHO MIKOA YA MTWARA, LINDI, SONGEA NA PWANI

Wakala wa Vipimo (WMA) imeendelea kufanya uhakiki na ukaguzi wa kushtukiza katika vituo vya kununulia Korosho katika Mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, na Pwani ambapo jumla ya Wilaya 20 katika Mikoa yote zilifikiwa. Zoezi la ukaguzi wa kushtukiza limefanyika katika Mikoa hiyo mwezi Novemba na Desemba 2018 baada ya kukamilika kwa zoezi la uhakiki wa Mizani zote zinazotumika katika ununuzi wa zao la Korosho na zoezi hilo hufanyika kabla ya kufunguliwa kwa msimu.

Akizungumza na Waandishi wa habari Meneja wa Vipimo Mtwara Bw. David Makungu amesema jumla ya vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS) 919 vilikaguliwa wakati wa kaguzi za kushtukiza na idadi ya mizani ya vyama vya Msingi 1,296 na mizani 20 ya kwenye maghala makuu (weigh bridge) ilikaguliwa. Katika ukaguzi huo uliofanyika mizani 23 zilibainika kuwa na makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na mizani kutokupima sahihi, mawe ya mizani kuongezewa uzito na baadhi ya mizani kutumiwa bila kuhakikiwa.

Meneja Makungu aliendelea kuzungumza kuwa katika ukaguzi huo uliofanyika kuna waliobainika kuwa na makosa mbalimbali ambapo Mizani ishirini na tatu (23) ilibainika kuwa na makosa na wamiliki wa mizani hiyo walikubali makosa yao na kufifilishwa, gharama za kufifilishwa huanzia shillingi laki moja (100,000/=) mpaka milioni ishirini (20,000,000/=) kwa kosa.

Vilevile watu wanne kati ya waliokamatwa walikana makosa yao hivyo kesi zao zipo mahakamani. Endapo watuhumiwa hao watakutwa na hatia kwa kosa la kwanza watuhumiwa watatozwa faini isiyopungua Shillingi 300,000/= na isiyozidi millioni 50 au kifungo kisichozidi miaka miwili (2) au vyote kwa pamoja, mujibu wa Sheria ya Vipimo sura na. 340 na mapitio yake ya mwaka 2002.

Pia, endapo mtuhumiwa atakamatwa na kosa kwa mara ya pili na kuendelea na akipelekwa Mahakamani akakutwa na hatia adhabu ni faini isiyopungua Shillingi 500,000/= na isiyozidi millioni 100 au kifungo kisichozidi miaka mitano (5) au vyote kwa pamoja.

Baadhi ya Wakulima wa zao la korosho katika wilaya ya Newala wameipongeza sana Serikali kwa kuweza kununua korosho zao, lakini pia wameipongeza wakala wa vipimo kwa kuhakikisha inasimamia usahihi wa vipimo (Mizani) inayotumika kununulia Korosho za Wakulima kwani wamenufaika na kupata faida kulingana na thamani ya Korosho walizouza.

Akimalizia Meneja Makungu ametoa wito kwa Wananchi wote kutojihusisha na uchezeaji wa Vipimo kwani kufanya hivyo ni wizi na dhuluma ya mali za wananchi na nikinyume na sheria ya vipimo na hata vitabu vya dini pia vinakataza.

Amewataka Wananchi wawe waangalifu wanapoenda kununua bidhaa mbalimbali na waweze kujiridhisha kama mizani walizopimiwa bidhaa zimehakikiwa na Wakala wa Vipimo na kuwekewa stika pamoja na alama ya Bibi na Bwana na tarakimu mbili za mwisho za mwaka husika mfano 2019 itasomeka (19).

Lakini pia, endapo mwananchi yeyote anakutana na changamoto ya vipimo nchi nzima tafadhali aweze kutupigia kwa kutumia namba ya simu ya bure ambayo ni 0800 11 00 97.