UMOJA WA VIWANDA VYA ALIZETI WAPATIWA ELIMU YA VIPIMO

Imewekwa:September 23, 2025

Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Dodoma imetoa wito na kuwahakikishia wafanyabiashara wa Mji wa Kibaigwa Wilayani Kongwa kusimamia usahihi wa vipimo vinavyotumika kufanyia biashara katika eneo hilo kwa lengo la kuhakikisha kunakuwa na biashara ya usawa na haki ili mnunuzi na muuzaji wapate bidhaa kwenye usawa kulingana na kiasi cha fedha kinachotumika.

Wito huo umetolewa na Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Dodoma Bw. Karim Zuberi alipokuwa akizungumza na umoja wa wenye Viwanda vya alizeti Kongwa (UVAKO) wakati wa semina ya matumizi sahihi ya vipimo kwa wafanyabiashara wa umoja huo siku ya tarehe 13 Septemba, 2025 kwenye mji wa Kibaigwa.

“Mji wa Kibaigwa ni miongoni mwa miji mikubwa yenye mzunguko mkubwa wa biashara na una idadi kubwa ya vipimo vinavyotumika katika eneo hili, Jukumu kuu la WMA ni kusimamia usahihi wa vipimo hivyo tutaendelea kufanya kaguzi za vipimo kila mara kama Sheria ya Vipimo Sura 340 inavyoelekeza ikiwa ni pamoja na kufanya kaguzi za kushtukiza mara kwa mara kwa lengo la kuhakikisha biashara zinafanyika kwa haki pasipo upande wowote kupunjika”. Amesema Meneja Zuberi.

Kadharika, akizungumza wakati wa uwasilishaji wa mafunzo kwa wana UVAKO Afisa Vipimo Mwandamizi Bw. Saidi Ibrahimu amewataka wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda vya alizeti kuhakikisha mizani inayotumiwa kununua na kuuza zao la alizeti imehakikiwa na WMA na imebandikwa stika inayoonyesha tarehe mzani uliyokaguliwa na tarehe ambayo utatakiwa kuhakikiwa tena.

Pia, Bw. Saidi Ibrahimu amewataka wafanyabiashara watakao ongeza thamani ya zao la alizeti kwa kukamua mafuta ya alizeti na kuyafungasha wazingatie matumizi sahihi ya vipimo kwa kuweka ujazo sahihi wa bidhaa hiyo kwenye vifungashio ili waepuke kujipunja na kuwapunja wanunuzi wa bidhaa hiyo.

“unapufungasha bidhaa kuna mambo muhimu ya kuzingatia ikiwa ni pamoja na kuweka jina la utambulisho wa bidhaa, jina na mahali unapofanyia ufungashaji, weka anuani ya posta, simu au barua pepe kwa ajili ya kurahisisha mawasiliano pamoja na kuandika kiasi cha bidhaa kilichofungashwa kwenye kifungashio na kuweka alama ya ujazo, uzito au urefu wa bidhaa mfano: 200 kg”. Amesema Bw. Saidi Ibrahimu.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Viwanda vya alizeti Kongwa (UVAKO) Bw. Clement Sangale ameipongeza Wakala wa Vipimo kwa kuwapatia elimu kuhusu matumizi sahihi ya vipimo kwani ilikuwa ni shauku yao muda mrefu kupata elimu hiyo ikiwa ni pamoja na kupitishwa katika Sheria ya Vipimo Sura 340 kwa lengo la kuifahamu ikiwa ni pamoja na kufahamu ada mbalimbali zinazotozwa na Wakala wa Vipimo.

“Semina hii imekuwa na manufaa makubwa kwa wajumbe wa UVAKO ambapo pamoja na mengine mengi tumefahamu haki na wajibu wetu kama wafanyabiashara hivyo tunaahidi kuendelea kutii sharia bila shuruti kwa kuzingatia matumizi sahii ya vipimo katika maeneo yetu ya biashara” Amesema Bw. Clement Sangale.

Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Dodoma Bw. Karim Zuberi ameelza kuwa moja ya majukumu ya WMA ni kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya vipimo hivyo, elimu hiyo ya vipimo itaendelea kutolewa katika makundi mbalimbali ya wafanyabiashara, wakulima na wananchi kwa ujumla. Meneja Zuberi ameeleza kuwa kwa sasa elimu ya vipimo iataelekezwa kwenye shule mbalimbali za Msingi na Sekondari kwa kuhakikisha wanafaunzi wanapata uelewa mzuri wa matumizi sahihi ya vipimo na litakuwa ni zoezi endelevu.