UMUHIMU WA KUTUMIA VIPIMO SAHIHI KATIKA SEKTA YA MADINI
Imewekwa:September 20, 2021
UMUHIMU WA KUTUMIA VIPIMO SAHIHI KATIKA SEKTA YA MADINI
Wakala
wa Vipimo (WMA) inawakaribisha wananchi wote wa Geita na Mikoa yote ya karibu
kuhudhuria katika maonesho ya nne ya Teknolojia na uwekezaji katika sekta ya
Madini ambayo yanafanyika katika viwanja vya EPZ bomba mbili mjini Geita. Lengo
kuu la Wakala wa Vipimo kushiriki katika maonesho haya ni kuwapa elimu Wananchi
kuhusu umuhimu wa kutumia Vipimo sahihi pamoja na kuhabarisha Umma kuhusu
majukumu ya Wakala wa Vipimo katika sekta mbalimbali hususani ya Madini.
Akizungumza
na mwandishi wetu Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Geita BW. Moses Ntungi amesema,
Serikali inaendelea kuiwezesha Taasisi ya Wakala wa Vipimo kwa kuinunulia
vitendea kazi vya kisasa kama vile mizani ya kupimia uzito wa madini pamoja na
mawe maalumu (standards) zinazotumika kuhakikia mizani katika masoko ya madini
na maduka ya kuuzia vito mbalimbali. Wakala wa Vipimo kupitia ofisi zake zote
Tanzania Bara hufanya uhakiki wa Vipimo kwenye masoko ya madini na maduka ya
kuuzia vito lakini kwa Mkoa wa Geita Wakala imefanya uhakiki wa Vipimo
katika masoko tisa kumi (10) ya
kuuzia na kununulia dhahabu ambayo ni Geita mjini, Katoro, Chato, Lwamgasa,
Nyarugusu, Mbogwe, Bukombe, Nyang’wale, Nyakagwe na Plant and Elution.
Meneja
Ntungi amesema kuwa, Wakala wa Vipimo inamchango mkubwa sana katika sekta ya
madini ambapo biashara hiyo haiwezi kufanyika bila kuwa na mizani sahihi na
iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo ili kuweza kutambua uzito halisi wa dhahabu
inayonunuliwa au kuuzwa. Jukumu kuu la Wakala wa Vipimo katika sekta hii ni
kuhakikisha mizani yote inayotumika kuuzia na kununulia vito na madini
inahakikiwa na inapima madini kwa usahihi na pia Taasisi hiyo inahakikisha
inatoa ushauri wa kitaalamu juu ya mizani zinazopaswa kutumika kuuzia madini
kwa kuwa siyo mizani yote inastahili kutumika kuuzia na kununulia madini.
Pia,
ameeleza kuwa mara baada ya uhakiki wa mizani hiyo kukamilika na kuanza
kutumika Wakala wa Vipimo hufanya zoezi la ukaguzi wa kushtukiza ili
kuhakikisha Vipimo vinatumika kwa usahihi kama inavyopaswa. Mara baada ya
kipimo kuhakikiwa na kubainika kipo sawa huwekewa alama maalumu (sticker) ya
Wakala wa Vipimo ambayo husaidia kutambua kuwa kipimo kimehakikiwa na kinafaa
kutumika kununulia madini na vito vya thamani. Aidha, alama zinazowekwa katika
mizani iliyohakikiwa ni hiyo stika pamoja na muhuri (stamp) ambayo inakuwa na
alama ya nembo ya taifa pamoja na tarakimu mbili za mwisho za mwaka husika
mfano (21) ikiashiria imehakikiwa 2021.
Vilevile,
ameeleza kuwa lengo na dhumuni la Wakala wa Vipimo kufanya uhakiki wa mizani ya
kuuzia na kununulia madini ni kuhakikisha matumizi ya mizani sahihi
iliyohakikiwa yanazingatiwa matakwa ya Sheria ya Vipimo na kunakuwa na biashara
ya usawa ambapo itawezesha Serikali kukusanya mapato kwa usahihi na wauzaji wa
madini wanapata fedha stahiki kulingana na thamani ya madini wanayouza.
Kadhalika, mara baada ya uhakiki wa mizani inayotumika kuuza na kununulia
madini Wakala wa Vipimo hufanya kaguzi za kushtukiza mara kwa mara katika
masoko ya kuuzia madini ili kujiridhisha kama mizani bado ipo sahihi na inaendelea
kutumika kwa usahihi kama inavyostahili.
Wakala
wa Vipimo inatoa wito kwa wafanyabiashara kutojihusisha na vitendo vya
uchezeaji wa vipimo kwa lengo la kutaka kujipatia faida zaidi kwani kufanya
hivyo ni kinyume cha Sheria ya Vipimo Sura Na. 340 ambayo inaeleza adhabu kwa
mtu atakaye kutwa amechezea vipimo ni faini isiyopungua shilingi laki moja
(100,000/=) na isiyozidi millioni ishirini (20,000,000/=) au kifungo
kisichozidi miaka mitano (5) au vyote pamoja faini na kifungo kwa kosa. Hivyo,
wito umetolewa kwa watumiaji wote wa vipimo kuzingatia matumizi sahihi ya
vipimo na wananchi kutembelea ofisi za Wakala wa Vipimo zilizopo katika mikoa
yote Tanzania Bara kwa ajili ya kupata ushauri wa kitaalamu kuhusu vipimo au
kutoa maoni na kuwasilisha malalamiko yao ili yaweze kufanyiwa kazi kwa lengo
la kuboresha utoaji huduma wa taasisi hiyo.
Pia,
wananchi wanakaribishwa kutumia namba ya simu ya bure ambayo ni 0800 11 00 97
endapo watakumbana na changamoto yeyote ya kivipimo na kitaalamu ili iweze
kufanyiwa kazi kwa wakati.