WAFANYABIASHARA WA SOKO LA MAWENZI MKOANI MOROGORO WAHIMIZWA KUTUMIA VIPIMO SAHIHI

Imewekwa:September 01, 2023

Meneja wa Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Morogoro Bw. Phanuel Matiko amewataka viongozi wa masoko ya Mkoa wa Morogoro na wafanyabiashara wa masoko yote hususani soko la Wakulima Mawenzi kuzingatia matumizi sahihi ya vipimo wakati wote na kujiepusha na matumizi ya vipimo batili ambavyo havikubaliki Kisheria kama makopo, visado na madebe kwenye uuzaji wa mazao na bidhaa mbalimbali.

Wito huo umetolewa kwenye kikao kilichofanyika kwenye soko la wakulima Mawenzi na kuwahusisha viongozi wa masoko ya Fire, Chamwino, Mazimbu, Kihonda Maghorofani, Nane Nane, Kingalu, Mji Mpya, Bigwa pamoja na wafanyabiashara wa soko la mawezi na viongozi wa Serikali za Mtaa.

Meneja Matiko ameeleza kuwa lengo la Wakala wa Vipimo ni kuhakikisha kunakuwa na usawa wakati wa ununuzi na uuzaji wa bidhaa mbalimbali kwa kuhakikisha muuzaji anapata pesa anayostahili na mnunuzi anapata bidhaa kulingana na thamani ya fedha yake pasipo kupunjwa. Kadhalika, amesisitiza kuwa Wakala wa Vipimo jukumu lake kuu ni kumlinda mlaji na kuhakikisha kunakuwa na mazingira wezeshi ya kufanya biashara pasipo kuwa na malalamiko kutoka upande wowote na sikukwamisha biashara kufanyika.

Vipimo batili maarufu kama visado, ndoo na Madebe vinaikosesha Serikali takwimu sahihi na vilevile havitendi haki kwakuwa visado vinatofautiana ujazo na hatua kali za Kisheria zitachukuliwa kwa wote watakao bainika kuendelea kuvitumia kama vipimo.

Matiko amesema ni muda wa wafanyabiashara kubadilika kwa kuanza kutumia mizani sahihi na iliyohakikiwa katika uuzaji wa bidhaa zao na wanunuzi kutokukubali kununua bidhaa bila kupimiwa kwenye mizani kila mara wanapoenda kupata huduma kwenye masoko.

Kwa upande wake Meneja wa Soko la Mawenzi Bw. Abdul Mkangwa amewataka wafanyabiashara wa soko hilo kutii Sheria bila shuruti na kuwahimiza wafanyabiashara wote wa soko hilo kuhakikisha wanakuwa na mizani sahihi iliyohakikiwa ili kujiepusha na usumbufu wa kutozwa faini pale wanapokutwa na makosa ya kutumia vipimo batili kwani kutumia vipimo hivyo ni kosa Kisheria.