WAKALA WA VIPIMO MKOA WA KIGOMA YAHIMIZWA KUENDELEA KUSIMAMIA MATUMIZI SAHIHI YA VIPIMO KWENYE MAWESE
Imewekwa:May 08, 2023
Kufuatia ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) aliyofanya Mkoa wa Kigoma akiwa na lengo la kuhamasisha kilimo cha mchikichi ambapo katika ziara hiyo aliagiza kutokomezwa kwa vipimo batili maarufu kama bidoo kwenye biashara ya mawese kwa kuwa vinawapunja wakulima wa zao hilo.
Katika
utekelezaji wa agizo hilo wakala wa vipimo imefanya kikao na viongozi
mbalimbali wa Mkoa wa Kigoma ambapo katika ufunguzi wa kikao hicho akizungumza
mgeni rasmi Mhe. Kanali Michael Ngayalina Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe ambaye
alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma amesema ni ukweli usiopingika kwamba
matumizi ya vipimo na udhibiti wake, hususani kwenye biashara ya mawese umekuwa
na changamoto nyingi.
Baadhi
ya changamoto hizo ni kukosekana kwa masoko/vituo rasmi vya kufanyia biashara
ya mawese kwenye maeneo mengi, hali inayotoa mwanga kwa wanunuzi kununua mawese
kwenye vinu vya uzalishaji na wakati mwingine kwenye nyumba za wananchi (wakulima)
wetu. Hali hii siyo tu kwamba inafanya kazi ya udhibiti wa matumizi ya vipimo
kuwa ngumu, bali huikosesha serikali (mamlaka zetu) sehemu ya ushuru pamoja na
kushindwa kupata takwimu sahihi za uzalishaji na mauzo ya mawese.
Kadhalika,
Mgeni rasmi Kanali Michael Ngayalina ameipongeza taasisi ya Wakala wa Vipimo
kwa kuendelea kusimamia matumizi ya vipimo kwenye maeneo mbalimbali ya biashara
na huduma pamoja hatua walizokwisha chukuwa kufikia sasa kudhibiti matumizi ya
BIDOO kwenye biashara ya mawese kwenye maeneo mbalimbali ya mkoa wetu ili
kuhakikisha biashara hiyo inafanyika kwa haki na usawa bila upande wowote
kupunjika na ameitaka Wakala wa Vipimo kusaidia upatikanaji wa vibaba vya
gharama nafuu ambavyo vitatumika kupimiwa mafuta ya mawese.
Akizingumza
wakati wa kikao Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Kigoma Bw. Laurent Kabikiye
ameeleza kuwa wakala wa Vipimo inatoa elimu mara kwa mara kuhusiana na madhara
ya kutumia vipimo batili (Bidoo) ili kuweza kumlinda mkulima wa zao la chikichi
na mnunuzi pia. Pamoja na elimu hiyo wakala wa vipimo inafanya jitihada za
kutafuta vipimo vitakavyo patikana kwa gharama nafuu (Kibaba) ambavyo vitakuwa
na ujazo mbalimbali ili kuwasaidia wafanyabiashara wa mawese kuweza kuuza
bidhaa zao kwa kutumia kipimo hicho ambacho ni sahihi ili kuwasaidia kupata
faida bila kupunjwa.
Katika
kikao hicho ambacho kilihudhuriwa na viongozi na watendaji mbalimbali wa Mkoa
wa Kigoma kama Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Kigoma, Makatibu Tawala
wasaidizi sekretariet ya Mkoa, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi watendaji
wa Halmashauri za Mkoa, Maafisa Tarafa, Maafisa Biashara kutoka Halmashauri
zote za Mkoa, Meneja wa SIDO na TBS pamoja na watumishi wa Wakala wa Vipimo.
Aidha,
washiriki wa kikao kazi hicho kwa pamoja wamekubaliana kuwa Halmashauri
zianzishe masoko (Buying Centres) za kuuzia na kununulia mawese pamoja na
kununua vipimo vilivyohakikiwa na Wakala wa Vipimo na kuhamasisha wauzaji wa
mawese kununua vipimo ili vitumike kununua na kuuzia mawese na kutokomeza
matumizi ya vipimo batili (Bidoo).