WAKALA WA VIPIMO MKOA WA KINONDONI YATOA ELIMU YA UFUNGASHAJI SAHIHI WA MAZAO KATIKA SOKO LA MABIBO GAMETS

Imewekwa:May 31, 2024

Katika kuendeleza mapambano dhidi ya lumbesa, Wakala wa Vipimo Mkoa wa Kinondoni imetoa elimu juu ya ufungashaji sahihi wa mazao kwa wafanyabiashara wa viazi katika soko la Mabibo Gamets.

Akitoa elimu hiyo, Afisa Vipimo Mwandamizi Bw.Renatus Mathayo amewajengea ufahamu juu ya Sheria na kanuni za vipimo zinazodhibiti ufungashaji wa mazao na kuepuka ufungashaji usiofuata sheria ujulikanao kama lumbesa.

“Ndugu wafanyabiashara, epukeni ufungashaji usiofuata sheria ujulikanao kama lumbesa. Ufungashaji huu una madhara makubwa kwa afya ya binaadamu (mbebaji), miundombinu yetu ya barabara, vyombo vyetu vya kusafirishia mazao hayo, pia lumbesa inaminya haki ya mkulima na inamdhulumu kwa sababu afungashapo mzigo wake, anafungasha kwa makadirio tu na sio kutumia mizani iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo. Kwa hiyo mkulima anakosa uwiano mzuri kati ya mzigo na pesa anayopata kutokana na mazao yake na hivyo kujikuta anapunjika na kunyonywa na mfanyabiashara. Kwa mujibu wa sheria ya vipimo sura Na.340, mazao yote yanatakiwa kufungashwa katika uzito wa kilogramu 100 na sio vinginevyo na kwa atakae kaidi atakutana na mkono wa sheria” amesema Bw.Renatus.

Kwa upande wake mwenyekiti wa soko la Mabibo Gamets Bw.Yusuph Kilema, ameshukuru Wakala wa Vipimo mkoa wa vipimo Kinondoni kwa kutoa elimu kwa wafanyabiashara sokoni hapo juu ya ufungashaji sahihi wa mazao hasa zao la viazi ambalo linauzwa sokoni hapo na
kuahidi kushirikiana na Wakala wa Vipimo katika kudhibiti ufungashaji holela wa mazao (lumbesa).

Katika mapambano dhidi ya “lumbesa”,Wakala wa Vipimo imejikita katika kutoa elimu kwa wadau na wananchi juu ya madhara yatokanayo na ufungashaji usio sahihi na kufanya kaguzi za mara kwa mara katika vyombo vya usafirishaji wa mazao,masokoni na maeneo mbalimbali ya ufungashaji wa mazao ili kudhibiti ufungashaji wa mazao usiofuata sheria ujulikanao kama lumbesa.