WAKALA WA VIPIMO NA EWURA ZAFANYA UKAGUZI KATIKA VITUO VYA KUUZA MAFUTA MKOANI PWANI

Imewekwa:May 13, 2024

Wakala wa Vipimo (WMA) imeshirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kufanya ukaguzi wa kushitukiza katika vituo mbalimbali vya kuuza mafuta mkoani Pwani.

Katika ukaguzi huo wa siku mbili, Wakala wa Vipimo (WMA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), zililenga kubaini vipimo vitumikavyo katika kupima mafuta (fuel pump) na usahihi wa matumizi ya vipimo hivyo katika kuwahudumia wateja.

Katika zoezi hilo, Wakala wa Vipimo (WMA) iliongozwa na Meneja wa Mkoa wa vipimo wa Ilala Bwana Muhono Nashon, ambae amesema kuwa, zoezi hilo la ukaguzi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) limekwenda vizuri na limefanyika kwa ufanisi mkubwa ambapo vituo kumi na moja kati ya 178 vya mafuta mkoani Pwani vimekaguliwa na kutoa matokeo mazuri katika ukaguzi huo jumuishi.

Bwana Nashon ameongeza kuwa, Wakala wa Vipimo inawaasa wananchi na wadau mbalimbali kuendelea kutumia vipimo sahihi katika upimaji ili kuleta tija na maendeleo kwa mtu binafsi na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, mkaguzi mwandamizi wa mafuta Mhandisi Emmanuel Panja ambae amewakilisha Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) katika ukaguzi huo jumuishi amesema kuwa, zoezi hilo limefanyika vizuri na kutoa taswira chanya kwa vituo vilivyokaguliwa na kuongeza kuwa EWURA itaendelea kushirikiana na Wakala wa Vipimo (WMA) katika kaguzi na oparesheni zijazo.

Wakala wa Vipimo kupitia sheria ya vipimo sura Na.340 hufanya kaguzi mbalimbali na endelevu katika maeneo ya biashara, afya, mazingira na uzalishaji ili kuhakiki vipimo vitumikavyo katika maeneo hayo na usahihi wa matumizi ya vipimo hivyo ili kusimamia haki na usawa kati ya mnunuzi na mtoa huduma.