WAKALA WA VIPIMO TANZANIA BARA (WMA) NA ZANZIBAR (ZAWEMA) ZAKUBALIANA KUSHIRIKIANA KUSIMAMIA MATUMIZI SAHIHI YA VIPIMO
Imewekwa:January 14, 2024
Taasisi za Wakala wa vipimo za Serikali ya Jamuhuri ya Muungano
wa Tanzania (WMA) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (ZAWEMA) zimetiliana
saini hati ya makubaliano ya ushirikiano (MoU) ili kuimarisha utendaji kazi wao
katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kubadilishana utaalamu na vitendea
kazi ili kuendelea kutoa huduma bora kwa Wananchi wanao hudumiwa kwa upande wa
Bara na Visiwani Zanzibar.
Akizungumza
mara baada ya kushuhudia utiaji saini huo katika Ukumbi wa Dokt Mwinyi kituo
cha maonesho ya biashara Nyamanzi Fumba Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na
Biashara Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Hashil Abdallah
amesema ni vyema kuimarisha mashirikiano kati ya taasisi hizo ili kuhakikisha
vipimo vyote vinakuwa sahihi na mnunuzi wa bidhaa anapata kulingana na thamani
ya fedha anayotoa.
Dkt. Hashil amesema,
kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo Wakala wa Vipimo ndio taasisi pekee inayopaswa
kusimamia matumizi sahihi ya vipimo kwa kuhakikisha kuwa vipimo vinavyotumika
katika biashara viko sahihi, na kuzingatia matumizi sahihi ya vipimo ili
kuepusha madhara yatokanayo na vipimo batili na kulinda walaji na watumiaji.
Aidha,
amesema makubaliano hayo yatasaidia kuimarisha utendaji wa kazi na kuongeza
ufanisi utakaopelekea kufikia malengo ya Taasisi hizo kwakuwa taasisi ya Wakala
wa Vipimo Bara (WMA) ilianzishwa muda mrefu na inauzoefu wa muda mrefu na vifaa
vingi vya kisasa kwa mashirikiano haya itaiwezesha zaidi taasisi ya ZAWEMA
kutumia pia vifaa hivyo na wataalamu ili kusimamia matumizi sahihi ya vipimo
katika sekta nyingi zaidi.
Kadhalika, Katibu Mkuu Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko
Zanzibar Ndugu. Ali Khamis Juma ameeleza kuwa mashirikiano baina ya taasisi za
WMA na ZAWEMA ni mashirikiano ya kudumu kwa muda mrefu sio ya kipindi cha muda
mfupi kwani hivyo itaiwezesha taasisi ya ZAWEMA kukua zaidi na kuingia katika
maeneo mengi ya kiutendaji kama ilivyo upande wa WMA Tanzania Bara.
Akizungumza na waandishi Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo
Bara (WMA) Bi. Stella Kahwa ameeleza kuwa mashirikiano baina ya WMA na ZAWEMA
yamekuwepo kwa muda japo hayakuwa rasmi kimaandishi na sasa yamekuwa rasmi
taasisi hizi zitazidi kuimarisha zaidi mashirikiano hayo na mara nyingi WMA na
ZAWEMA hushirikiana hata katika kuendesha kaguzi mbalimbali visiwani Zanzibar kwa
wauzaji wa vito na madini, mafuta na hata katika sekta ya gesi ili kuhakikisha
vipimo vinakuwa sahihi wateja hawapunjiki.
Kwa upande
wake Mkurugenzi wa wakala wa Vipimo Zanzibar (ZAWEMA) Bw. Mohammed Simai Mwalim
ameeleza kuwa endapo vipimo vitasimamiwa kwa usahihi katika bidhaa mbalimbali
zinazozalishwa nchini na bidhaa zinazoingizwa kutoka nje ya nchi itasaidia
Serikali kukusanya kodi kwa usahihi.
Hata hivyo
alisema endapo vipimo hivyo havitasimamiwa vyema itasababisha wananchi kupata huduma
au bidhaa ambazo haziendani na thamani ya fedha wanayotumia.
Mkurugenzi
Mohammed ametoa wito kwa wananchi na wafanyabiashara wote wa Tanzania bara na
Zanzibar kuhakikisha wanatumia vipimo sahihi na endapo watakutana na changamoto
yoyote inayohusu vipimo wafike kwenye ofisi za Wakala wa Vipimo kwa ajili ya
kupata msaada wa kitaalamu.
Hata hivyo
aliwaonya Wamiliki wa vipimo kutochezea vipimo kwa lengo la kuwaibia wananchi,
kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria na hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wote
watakaobainika kufanya vitendo hivyo ambavyo vinakatazwa hata kwenye maandiko
matakatifu.
Nao Washiriki
walioshuhudia utiaji wa saini huo walisema kuwa makubaliano hayo yametiwa saini
katika kipindi muafaka cha kuadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi na yataongeza
mashirikiano zaidi ili kuyaenzi na kuyalinda Mapinduzi hayo.
Hati hiyo ya
makubaliano ya kiutendaji yalisainiwa na Mtendaji Mkuu wakala wa vipimo Bara
(WMA) Stela Kahwa na kwa upande wa Zanzibar Mkurugenzi wakala wa vipimo
Zanzibar (ZAWEMA) Mohammed Mwalim Simai.