WAKALA WA VIPIMO (WMA) MKOA WA TEMEKE YATOA ELIMU KWA WAFANYABIASHARA SOKO LA STEREO

Imewekwa:May 18, 2024

Kuelekea Siku ya Vipimo Duniani ambayo huadhimishwa Mei 20 kila mwaka, Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Temeke imetoa Elimu ya Vipimo kwa wafanyabiashara na wadau wa vipimo wanaofanya shughuli zao katika Soko la Stereo- Temeke, Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na wawakilishi wa wafanyabiashara sokoni hapo, Meneja wa Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Temeke Bwana Gasper Matiku amesema kuwa, lengo la ziara ya Wakala wa Vipimo sokoni hapo ni kukumbushana juu ya matumizi sahihi ya vipimo katika Nyanja mbalimbali ili kuendelea kujenga uelewa sahihi wa vipimo kwa wafanyabiashara.

Aidha, Bwana Matiku amewahimiza wafanyabiashara wa mazao ya shambani kutumia mizani katika upimaji wa mazao hayo badala ya kupima kwa njia ya mafungu, kwani matumizi ya mizani huleta matokeo yaliyosahihi na yenye usawa kwa mnunuzi na muuzaji.

“Tutengeneze urafiki, tufuate sheria, tuzingatie utaratibu uliowekwa na Serikali yetu na Dunia kwa ujumla, ikiwa kuna changamoto yoyote tukae tuzungumze tuelekezane, hakuna hasara yeyoye anayopata mfanyabiashara anayetumia vipimo kwa usahihi” Amesema Bwana Matiku.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Soko la Stereo-Temeke, Bwana Rashidi Milao, ameipongeza Wakala wa Vipimo kwa kuwakumbusha wafanyabiashara umuhimu wa kutumia vipimo sahihi kwani kupata elimu hiyo kutawafanya watambue wapi walikua wanakosea na waanze kutumia vipimo kwa usahihi.

Bwana Milao ameiomba Wakala kuendelea kutoa Elimu kila mara kwa wafanyabiashara na kuhimiza mashirikiano chanya kati ya Wakala na Wafanyabiashara.

Wakala wa Vipimo (WMA) inaendelea kujikita katika kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya vipimo na kuwafikia wadau katika maeneo mbalimbali ili kuwajengea ufahamu juu ya masuala mbalimbali ya vipimo, Wakala wa Vipimo (WMA) pamoja na taasisi zingine za vipimo za kikanda na duniani kote zitaadhimisha siku ya vipimo duniani tarehe 20 Mei mwaka huu, huku kauli mbiu ikiwa ni “tunapima leo kwa kesho endelevu”