WAKALA WA VIPIMO (WMA) YASHIRIKI KUTOA ELIMU SOKO LA KARUME MACHINGA COMPLEX
Imewekwa:May 18, 2024
Kuelekea katika maadhimisho ya siku ya Vipimo Duniani,Wakala wa vipimo (WMA) imeshiriki katika kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya vipimo kwa wafanyabiashara wa soko la karume machinga complex wilayani ilala Jijini Dar es salaam.
Akitoa
elimu hiyo katika mkutano wa robo ya tatu ya mwaka kwa wafanyabiashara hao,
meneja wa mkoa wa vipimo wa ilala Bwana Mhono Nashon, amewajengea ufahamu wa
namna ya kutumia vipimo sahihi vilivyo hakikiwa na Wakala wa Vipimo katika
maeneo yao ya biashara ili kuleta usawa baina ya mfanyabiashara na mnunuzi.
Bwana
Nashon ameongeza kuwa wakala wa vipimo itaendelea kuwatembelea wadau mbalimbali
katika maeneo yao ya biashara na kuwapa elimu juu ya masuala mbalimbali ya
vipimo ili kuondokana na ufanyaji biashara usiozingatia sheria na taratibu za
vipimo.
“Tunatakiwa
kutumia vipimo sahihi na vilivyohakikiwa na Wakala wa Vipimo ili kuepuka
madhara yatokanayo na upimaji usiozingatia taratibu na sheria za vipimo, natoa
rai kwa wafanyabiashara katika soko hili la karume machinga complex, kuondokana
na upimaji wa kimazoea kwa kutumia mafungu, visado, vifungashio na vipimo
vinginevyo batili kwani hii inadumaza ustawi wa biashara, lakini pia
kutengeneza uwiano usio sawa baina ya mfanyabiashara na mteja na hivyo kudumaza
maendeleo ya taifa katika Nyanja mbalimbali” amesema Bwana Nashon.
Kwa
upande wake meneja wa soko hilo Bi.Stella Mgumia, ameishukuru Wakala wa Vipimo
kwa ushiriki wake katika mkutano huo na wafanyabiashara sanjari na kutoa elimu
ya matumizi sahihi ya vipimo katika maeneo mbalimbali ya biashara.
Bi.
Mgumia amesema kuwa, wafanyabiashara katika soko la karume machinga complex
wameahidi kutumia vipimo sahihi katika maeneo yao ya biashara na kutoa
ushirikiano kwa wakala hiyo katika kazi zake.
Wakala
wa Vipimo (WMA) inaendelea kujikita katika kutoa elimu juu ya matumizi sahihi
ya vipimo na kuwafikia wadau katika maeneo mbalimbali ili kuwajengea ufahamu
juu ya masuala mbalimbali ya vipimo. Wakala hii inaendelea kuchangamana na
wananchi na wadau katika muundo chanya kwa nyakati mbalimbali huku ikijiandaa
na maadhimisho ya siku ya Vipimo Duniani ambayo hufanyika Mei 20 ya kila mwaka.
Wakala wa Vipimo (WMA) na taasisi zingine za vipimo za kikanda na duniani kote zitaadhimisha siku ya vipimo duniani huku kauli mbiu ikiwa ni “tunapima leo kwa kesho endelevu”.