WAKALA WA VIPIMO (WMA) YASISITIZA MATUMIZI SAHIHI YA VIPIMO KATIKA MAONESHO YA SABASABA
Imewekwa:July 08, 2024
Wakala wa Vipimo (WMA) inaungana na taasisi zingine katika kushiriki maonesho ya 48 ya kimataifa ya biashara ya Dar es Salaam (SabaSaba) yanayofanyika katika viwanja vya SabaSaba wilayani Temeke Jijini Dar es Salaam.
Katika
maonesho hayo, Wakala wa Vipimo inajikita katika kutoa elimu ya matumizi sahihi
ya vipimo katika maeneo mbalimbali ya biashara, afya, mazingira na usalama,
kutoa ushauri wa kitaalamu juu ya masuala mbalimbali ya kivipimo, kuwajengea
ufahamu wadau na wananchi kwa ujumla juu utendaji kazi wa WMA katika uhakiki wa
Mita za Umeme, Dira za Maji na vipimo vingine mbalimbali.
Katika
namna ya kipekee, WMA pia inaendelea kutoa elimu kwa wadau na wananchi kwa ujumla juu ya
ufungashaji sahihi wa mazao katika uzito wa kilogramu 100 kama Sheria ya Vipimo
Sura Na. 340 inavyoelekeza na wajiepushe kufungasha mazao ya shamba kwa uzito
unaozidi kiligramu 100 maarufu kama Lumbesa kwani kufungasha hivyo ni kosa
kisheria.
Kadharika,
Wakala wa Vipimo inaendelea kutoa elimu kwa wauzaji wa mazao mbalimbali kuuza
kwa kutumia mizani sahihi iliyohakikiwa na siyo kwa kutumia makopo, visado na
ndoo na wito unatolewa kwa wanunuzi wote wa bidhaa kutumia mizani katika manunuzi yao yote
katika masoko na maduka ya kuuzia bidhaa.
Aidha,Wakala
wa Vipimo inawakaribisha wadau wa vipimo na wananchi wote kutembelea banda lake lililopo
ndani ya banda la Wizara ya Viwanda na Biashara katika viwanja vya SabaSaba ili
kuweza kujipatia elimu na ushauri wa kitaalamu juu ya masuala mbalimbali ya
vipimo.
Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) yamefunguliwa Rasmi Julai 3, 2024 na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji Mhe. Filipe Jacinto Nyusi ambaye aliambatana na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.