WAFANYABIASHARA WA MBOGA MBOGA WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA YA VIPIMO

Imewekwa:March 08, 2024

Afisa mtendaji mkuu Wakala wa Vipimo( WMA) Bi. Stella Kahwa, amekutana na kufanya mazungumzo na wafanyabiashara wa mboga mboga na matunda (WAMBOMADA) katika ukumbi wa mikutano wa Wakala wa Vipimo Makao Makuu,jijini Dar es Salaam.

Bi. Stella Kahwa, alifungua kikao na wafanyabiashara hao kwa kupokea barua kutoka kwa katibu wa WAMBOMADA Bw. Nabahani Fadhili, yenye vifungu kadhaa vya maombi ya ubadilishaji wa Sheria na utaratibu wa ufungashaji wa mazao katika gunia kwa uzito wa zaidi ya kilogramu 100.

Akiwasilisha hoja hizo, katibu mkuu wa wafanya biashara wa mboga mboga na matunda jijini Dar es Salaam (WAMBOMADA) Bw. Nabahani Fadhili, amesema kuwa wafanyabiashara hao wamekuwa wakipata hasara endelevu kutokana na ongezeko la tozo, ushuru, gharama za usafirishaji na gharama za ukusanyaji wa mazao kutoka shambani hadi kufika sokoni na maeneo ya biashara.

Bwana Nabahani ameongeza kuwa biashara hiyo ya matunda na mboga mboga imechukua taswira mpya baada ya Wakala wa Vipimo (WMA) kushinikiza na kusimamia vilivyo sheria na kanuni za ufungashaji wa mazao, ambazo zinamtaka mfanyabiashara kufungasha mazao kwa uzito usiozidi kilogramu 100.

Bwana Nabahani amekiri kuwa wafanyabiashara hao wanafahamu na kuifuata sheria ya vipimo inayomtaka mfanyabiashara kufunga mzigo usiozidi kilogram 100, lakini wamekuwa wakipata hasara za mara kwa mara kutokana na ufungashaji huo unaofuata sheria.

“Awali tulikuwa tunafunga mzigo mmoja mazo haya ya mboga mboga wenye kilogram 300, tulikuwa tunausafirisha kwa bei ya maelewano na tuliweza kulipia gharama za usafirishaji,tozo na ushuru kwa awamu moja, hii ilitufanya tupate unafuu katika biashara zetu. Lakini ufungashaji huu wa kisheria wa kilogram 100 kwa mzigo mmoja, unaleta changamoto kwa sababu inatupasa tufunge mizigo mingi ya kilogram 100 na kuilipia ushuru na tozo mara mbili au tatu zaidi na pia gharama za usafirishaji nazo zinakuwa kubwa kwani madereva wanatutoza pesa mara mbili ya kawaida kwa mizigo hii ya kilogram 100 na hata hivyo mara zote sehemu kubwa ya mzigo hii ya mboga mboga huaribikia safarini kwa hiyo katika kilogram 100, tunaweza kuambulia kilogram 70 tu ambazo tunaweza kuzifanyia biashara. Hii husababisha changamoto na hasara kubwa isiyo epukika. Rai yetu kwa Wakala wa Vipimo ni kwamba, tunaomba itizame hili na ikiwezana tunaomba mturuhusu tuweze kufunga mzigo angalau wa kilogramu 150 ili tuweze kufidia hasara hizi tunazopata” alisema Bwana Nabahani.

Akijibu hoja hizo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo Bi. Stella Kahwa, amewataka wafanyabiashara hao kuzingatia na kufuata sheria na kanuni za vipimo ambazo zinamtaka mfanya biashara kufunga mzigo wa mazao usiozidi kilogramu 100 kwani sheria hizi zimetungwa na Bunge na kusimamiwa vilivyo na Wakala wa Vipimo (WMA).

Bi. Stella ameongeza kuwa sheria hizi za vipimo zimewekwa kwa kuzingatia maslahi mapana ya kiuchumi, mazingira, miundo mbinu, na afya za pande zote husika katika biashara na hivyo kumlinda mlaji na kusimamia haki na usawa katika biashara hizo.

Sanjari na hayo, Bi. Stella Kahwa amepokea vyema ujumbe huo wa wafanyabiashara wa mboga mboga na matunda Dar es Salaam na kuahidi kushirikiana nao vyema na kusisitiza kuwa Wakala wa Vipimo itaendelea kutoa elimu na kusimamia vyema sheria ya vipimo katika wigo mpana zaidi.

Wakala wa Vipimo imekuwa ikikutana mara kwa mara na wadau, wafanyabiashara na watumiaji mbali mbali wa vipimo na kuwapa elimu, ushauri wa kitaalamu na uangalizi wa karibu ili kuwajengezea uwezo na kuhimiza matumizi sahihi ya vipimo.