WAKALA WA VIPIMO YA ADHIMISHA SIKU YA VIPIMO DUNIANI KWA KUGAWA MIZANI SOKO LA ILALA.

Imewekwa:May 31, 2024

Wakala wa Vipimo (WMA) imeungana na taasisi zingine za vipimo duniani kuadhimisha Siku ya Vipimo ambayo huadhimishwa Mei 20 kila mwaka.

Wakala wa Vipimo imeadhimisha siku ya vipimo duniani (World Metrology Day) kwa kutembelea soko la ilala na kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya vipimo katika maeneo mbalimbali ya biashara sanjari na kugawa mizani iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo kwa makundi ya wafanya biashara sokoni hapo.

Akimuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe.Edward Jonas Mpogolo katika hafla ya utoaji elimu na ugawaji wa mizani ilyofanyika sokoni hapo,Katibu Tawala wa wilaya hiyo Bi.Charangwa Seleman Makwiro ameipongeza Wakala wa Vipimo kwa kuwa na utaratibu wa kuwatembelea wadau na wafanya biashara na kuwapa elimu juu ya matumizi sahihi ya vipimo katika maeneo yao ya biashara.

Aidha,Bi.Charangwa amewaasa wafanya biashara sokoni hapo kujenga tabia endelevu ya kutumia mizani iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo katika biashara zao ili kuepuka madhara yatokanayo na matumizi yasiyo sahihi ya vipimo.

“ Ndugu zangu wafanyabiashara, upimaji wa bidhaa zenu kwa kutumia visado ambavyo mnaviita take away, na vipimo vingine vya mafungu na hata vifungashio, sio vipimo halali na vya uhakika, tunatakiwa tutumie vipimo sahihi kama vile mizani iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo ili kuepuka kujiibia na kupata hasara pamoja na kudumaza hali ya biashara zetu. Nawaasa mkiwa na jambo lenu mnahitaji utatuzi ofisi za Wakala wa Vipimo zipo, nendeni mtashughulikiwa na kutatuliwa shida zenu zote zinazohusu matumizi sahihi ya vipimo” amesema Bi.Charangwa.

Sanjari na hayo Bi.Charangwa ameshiriki kugawa mizani iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo kwa baadhi ya makundi ya wafanya biashara ili kuwasaidia katika shughuli mbalimbali za biashara na kuleta chachu ya matumizi sahihi ya vipimo katika maeneo ya biashara.

Naye Meneja wa Mkoa wa Vipimo wa Ilala Bwana Mhono Nashon ametoa elimu juu wa matumizi sahihi ya vipimo na kujibu hoja mbalimbali zilizowasilishwa kwake na wafanyabiashara.

Bwana Nashon amewataka wafanya biashara kujenga utamaduni wa matumizi sahihi ya vipimo na kuondokana na upimaji holela wa bidhaa kwani upimaji huo unafifisha ustawi wa biashara na kudumaza maendeleo ya taifa.

“ Ofisi yetu ya Wakala wa Vipimo Mkoa wa Ilala ilifanya utafiti mdogo tu wa kivipimo, tulinunua karoti, tulipimiwa kwa kutumia visado tofauti ambapo tulipopeleka kwenye vipimo tulikuta kisado kimoja kina kina kilogram 3.8 na kingine kina kilogram 4, sasa hapa utaona ni jinsi gani mfanya biashara anavyojidhulumu” amesema Bwana Nashon

Kwa upande wake mwenyekiti wa wafanya biashara wa soko la Ilala Bwana Ali Karimu Mbiku, ameshukuru Wakala wa Vipimo (WMA) kwa kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya vipimo pamoja na kuwapa mizani iliyohakikiwa na Wakala hiyo.

Bwana Mbiku ameiomba Wakala kuendelea kushirikiana na wafanya biashara na kuwapa elimu na kuwakumbusha mara kwa mara juu ya matumizi sahihi ya vipimo na kuchochea maendeleo ya taifa.

Wakala wa Vipimo na taasisi zingine za vipimo duniani zinaadhimisha siku ya vipimo ambayo hufanyika Mei 20 kila mwaka ikiwa ni kumbukizi ya mkataba wa kimataifa uliosainiwa mwaka 1875 Jijini Paris, nchini Ufaransa. Mkataba huo ulisainiwa na mataifa 17 kwa lengo la kuweka mfanano na usawa wa vipimo duniani ambapo Tanzania ilisaini mkataba huo Julai 17, 1964. Maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani mwaka huu yamepambwa na kauli mbiu isemayo “tunapima leo kwa kesho endelevu”