WAKALA WA VIPIMO YAENDELEA KUTOA ELIMU KUHUSU MIZANI KWA WAKULIMA WA PAMBA
Imewekwa:April 22, 2018WAKALA WA VIPIMO YAENDELEA KUTOA ELIMU KUHUSU MIZANI KWA WAKULIMA WA PAMBA
Wakala
wa Vipimo (WMA) inaendelea na zoezi la utoaji elimu kwa Wakulima na wadau wa
zao la pamba katika Mikoa saba (7) ya Kanda ya Ziwa ambayo ni Mwanza, Geita,
Simiyu, Tabora, Shinyanga, Mara pamoja na Kagera. Jumla ya wilaya 27 zitapata
elimu ya Mizani sahihi zinazotakiwa kutumika wakati wa msimu wa kuuza pamba.
Lengo
kuu la kutoa elimu kwa Wakulima kuhusu
Mizani sahihi zinazopaswa kutumika katika msimu wa ununuzi wa pamba, ni
kumlinda Mkulima ili apate fedha anayostahili kulingana na uzito wa pamba
anayoiuza, pia kuhakikisha mkulima anajua mambo muhimu ya kuzingatia ili kumuwezesha
kutambua mizani sahihi na zilizo hakikiwa na pia kuweza kutambua kwa urahisi
mizani zilizochezewa au kuharibiwa/kuharibika
Zoezi
hili la elimu ya Mizani kwa Wakulima wa pamba ni zoezi endelevu ambalo hutolewa
na Wakala wa Vipimo kila mwaka kabla ya kuanza kwa msimu wa ununuzi wa zao hilo,
na mpaka sasa zaidi ya mizani 626 imeanza kuhakikiwa tayari kwa maandalizi ya
msimu wa ununuzi wa pamba.
Mara
baada ya zoezi la elimu kukamilika kwa Wakulima wa pamba WMA itaingia katika
zoezi la awamu ya pili, ambalo ni operation
maafisa vipimo watapita katika vituo vya ununuzi wa pamba na kufanya kaguzi za
kushtukiza ili kuhakiki usahihi wa mizani zinazotumika na zinavyotumika.
Mkulima
wa pamba ataweza kutambua mizani zilizohakikiwa na Wakala wa Vipimo kwa
kuzingatia vitu vifuatavyo; Kwanza, Mizani zilizo hakikiwa zinakuwa na lakili (seal) yenye ngao ya taifa pamoja na
tarakimu mbili za mwisho za mwaka husika ambapo kwa mwaka 2018 itasomeka (18).
Pili,
mizani zilizohakikiwa zinakuwa na stika maalum ya WMA ambayo inaonesha tarehe
mizani iliyokaguliwa na tarehe ya mwisho kutumika, Vilevile Mkulima anatakiwa
kuhakikisha kuwa mizani inasoma sifuri (0) kabla hajaweka pamba yake kwa ajili
ya kuipima.
Kwa
mujibu wa Sheria ya Vipimo sura na. 340 na mapitio yake ya mwaka 2002 imeelezea
faini za makosa mbalimbali ambapo kwa mkosaji wa kosa la awali akipelekwa
Mahakamani akakutwa na hatia adhabu ni faini isiyopungua 300,000 na isiyozidi
millioni 50 au kifungo kisichozidi miaka miwili (2) au vyote kwa pamoja.
Vilevile,
endapo mchezea vipimo atakamatwa na kosa kwa mara ya pili na kuendelea na
akipelekwa Mahakamani akakutwa na hatia adhabu ni faini isiyopungua 500,000 na
isiyozidi millioni 100 au kifungo kisichozidi miaka mitano (5) au vyote kwa
pamoja.
Pia,
endapo mtuhumiwa atakamatwa na kukubali kosa lake basi atafifilishwa ambapo
faini yake ni kiasi cha fedha kisichopungua 100,000 na isiyozidi millioni 20.
Wakala
wa Vipimo inatoa wito kwa wadau wote wa zao la pamba kujiepusha na vitendo vya
udanganyifu wa aina yeyote haswa uchakachuaji wa mizani wakati wa ununuzi wa
pamba, kwani kwa yeyote atakaye kamatwa kwa makosa hayo atashitakiwa kwa mujibu
wa sheria.
Pia, WMA ina namba maalumu kwa ajili ya wananchi kupiga na kupata msaada pindi wakutanapo na changamoto za kivipimo, namba hiyo ni 0800 110097 namba hii ni bure kabisa.