WAKALA WA VIPIMO YAFANYA UKAGUZI WA KUSHTUKIZA KIBAIGWA
Imewekwa:August 08, 2025
Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Dodoma imefanya ukaguzi wa kushtukiza wa mizani inayotumika kununulia na kuuzia mazao katika Soko Kuu la mazao la kimataifa Kibaigwa kwa lengo la kujiridhisha kama mizani hiyo inafanya kazi kwa usahihi tangu ilipofanyiwa uhakiki na pia kujiridhisha kama mizani hiyo inatumika kwa usahihi.
Ukaguzi huo umefanyika katika kipindi cha maonesho ya Nane Nane ikiwa ni sehemu ya utoaji huduma kwa wakulima ili kuhakikisha wanapata faida kulingana na kiasi sahihi cha mazao wanachouza pasipo kupunjika pamoja na kuhakikisha mnunuzi wa mazao analindwa ili apate kiasi sahihi cha mazao anayonunua.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo la ukaguzi, Afisa Vipimo Mwandamizi Bw. Said Ibrahim alisema kuwa takribani mizani 55 zimehakikiwa katika zoezi hilo na mizani nyingi zilikuwa sahihi kasoro chache ambazo zilibainika kuwa na mapungufu na zimefanyiwa marekebisho kwa ajili ya kuendelea na shughuli za ununuzi na uuzaji wa mazao katika soko hilo.
Ukaguzi wa kushtukiza ni zoezi endelevu ambalo hufanyika baada ya kukamilika kwa uhakiki wa mizani ambapo utekelezaji wake ni kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo Sura Na. 340.
Ukaguzi hufanyika angalau mara moja kwa mwaka na mizani ambayo hukidhi vigezo huwekewa ulinzi wa alama za serikali ambazo ni stika pamoja na kufungwa lakiri (seal) yenye nembo ya Bibi na Bwana pamoja na kuwekewa tarakimu mbili za mwisho za mwaka husika mfano, 25.
“Wakala wa Vipimo itaendelea kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wafanyabiashara wanaofanya udanganyifu wa vipimo kwa lengo la kuwapunja wakulima,” amesisitiza Bw. Ibrahim na ametoa rai kwa wakulima kujiridhisha kama mizani imehakikiwa kabla ya kupima mazao yao.
Aidha, alifafanua kuwa kwa mizani za digitali mkulima anapaswa ahakikishe kabla ya kuanza kupima, mizani inasoma sifuri (0) na baada ya kushusha mzigo irudi kusoma sifuri isiweke alama ya hasi (-).
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Soko hilo la Kibaigwa Bw. Emmanuel Joachim alisema kuwa viongozi wa soko wanawahimiza wafanyabiashara mara kwa mara kutumia mizani iliyohakikiwa katika ununuzi na uuzaji wa mazao na wanapobaini kuna vitendo vya uchezewaji wa vipimo hutoa taarifa katika ofisi ya WMA Dodoma ili kuhakikisha haki inatendeka wakati wote na kuhakikisha mkulima na mfanyabiashara wanapata wanacho stahili.