WAKALA WA VIPIMO YAHIMIZA UFANYAJI KAZI KWA KUZINGATIA SHERIA YA VIPIMO
Imewekwa:April 12, 2022
Meneja wa Survaillance Bw. Almachius Pastory ambaye alimuwakilisha Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu amefanya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Mafundi Mizani ambao kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kakwe umefanyika Jijini Dodoma kwenye ukumbi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE).
Akizungumza kwa niaba
ya Afisa Mtendaji Mkuu Bw. Almachius Pastory ameeleza kuwa anafarijika sana kuona mafundi wanakuwa na
chama ambacho kinazingatia matakwa mbalimbali ya kisheria na miongozo
inayotolewa na Serikali hususani swala la uadilifu kwa wadau wa Vipimo ili
kupunguza malalamiko kwa Wananchi.
Pia, ameeleza kuwa Viongozi
watakao pata nafasi ya kuchaguliwa kuongoza chama hicho watakuwa msaada mkubwa
kwetu sote na Taifa kwa ujumla kwani ni viunganishi muhimu kati ya Wakala wa
Vipimo na Mafundi wote wanaojishughulisha na urekebishaji na uundaji wa mizani
na ukizingatia tunatumia vipimo kufanikisha mambo mbalimbali yanayotuzunguka
iwe kwenye ujenzi, Afya, Mazingira, Usalama na katika maeneo yote
yanayotuzunguka ya kibiashara.
Kadharika, ameeleza
kuwa kipimo ni nyenzo muhimu katika kubadilisha bidhaa na fedha ili biashara
ifanyike kwa haki lazima Vipimo sahihi vitumike na muundaji wa Vipimo lazima
aunde kipimo chenye usahihi vivo hivyo mrekebishaji wa Vipimo lazima ahakikishe
Vipimo vyote vilivyorekebishwa vinakidhi matwakwa ya Sheria ya Vipimo Sura na.
340. Kipimo kisichokidhi matakwa ya kisheria kinaweza kuzidisha au kupunguza
uzito wa bidhaa, kuzidisha kunampa hasara mwenye mali au duka na kumfanya asipige
hatua katika biashara yake. Kadharika, kupunguza kunasababisha mnunuzi kupata
bidhaa pungufu kulinganisha na pesa aliyoitoa.
Vilevile, amewataka
mafundi vipimo kuzingatia maadili ya kazi ya ufundi mizani ili kuepukana na adhabu
ya faini au vifungo kama Sheria ya Vipimo inavyosema, uzingatiaji wa Sheria
utaimarisha uaminifu kwa wateja hivyo kuongeza wigo wa kazi. Takwimu zilizopo
zinaonesha kuwa mafundi mizani wenye leseni kwa mwaka huu mpaka sasa ni 274
ambapo asilimia 40 wapo mkoa wa Dar es Salaam. Hivyo, nichukue nafasi hii
kuwahimiza kufungua Ofisi mikoani kwani huko pia wananchi wanahitaji sana
huduma zenu kwakuwa kuna Mikoa inaonekana haina fundi hata mmoja jambo ambalo
sisawa.
Kwa kumalizia Bw.
Pastory kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu ametoa wito kwa mafundi vipimo
kujiendeleza kitaaluma ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia kwakuwa
tunakoelekea vipimo vya kidigitali vitachukua nafasi kubwa zaidi ya hivi
vinavyotumika sasa hivyo, bila kujiendeleza kazi zetu tutajikuta zinafanywa na
wageni kwakuwa hakuna wataalamu wa kuweza kufanya kazi hizo nchini kwetu.