WAKALA WA VIPIMO YAPONGEZWA KUTOA ELIMU YA VIPIMO SONGEA
Imewekwa:August 26, 2021Mwakilishi
wa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Pololet Kamando Mgema ambaye ni Mkuu wa Wilaya
ya Songea ameipongeza taasisi ya Wakala wa Vipimo (WMA) kwa kutoa mafunzo ya
matumizi sahihi ya Vipimo na namna bora ya kuzingatia ufungashaji sahihi wa
bidhaa kwa Wafanyabiashara, Wajasiriamali na Wakulima wa Mkoa wa Ruvuma na
ameitaka taasisi hiyo kuendelea kuwasaidia wafanyabiashara kwa kuwapa elimu ya
vipimo mara kwa mara na kufanya kaguzi za kushtukiza ili kujiridhisha kama
vipimo vinatumika kwa usahihi.
Kadhalika Mhe. Pololet Kamando Mgema ameipongeza
Wakala wa Vipimo kwa kuongeza na kupanua wigo wa kazi za vipimo katika maeneo
mapya ambapo kwa sasa taasisi hiyo inafanya uhakiki wa dira za maji pamoja na mita
za umeme, kwa kuzingatia hilo Mhe. Pololet ameagiza Mamlaka zote za maji Mkoa
wa Ruvuma Ruwasa na Souwasa kuhakikisha wateja wote wanafungiwa mita za maji
zilizohakikiwa na Wakala wa Vipimo.
Vilevile, amewaonya wafanyabiashara wa Mkoa wa Ruvuma
kuacha tabia ya kutumia vipimo batili kama ndoo, dumla, lita, makopo na visado
na badala yake watumie mizani sahihi ambayo imehakikiwa na Wakala wa Vipimo
kwani kwa kufanya hivyo itawasaidia kutojipunja na wao kutowapunja wateja wao
hivyo kujenga uaminifu Zaidi katika biashara. Mhe. Pololet Mgema ameyasema hayo
jana wakati akifungua mafunzo na elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya
Vipimo na ufungashaji kwa wafanyabiashara wa Mkoa wa Ruvuma yaliyofanyika
katika ukumbi wa Manispaa ya Songea.
Akiwasilisha mada mtaalamu kutoka Wakala wa Vipimo Bi.
Rehema Michael aliwaeleza wafanyabiashara hao kuwa
Wakala wa Vipimo ni Wakala ya Serikali ambayo inatekeleza majukumu yake kwa
mujibu wa Sheria ya Vipimo Sura Na. 340 (mapitio ya mwaka 2002). Lengo la
Wakala wa Vipimo ni kumlinda mlaji na umma kwa ujumla kwa kufanya yafuatayo: Kuhakiki
vipimo vinavyotumika kwenye Sekta za Biashara, Afya, Usalama na Mazingira,Kudhibiti
matumizi yasiyo sahihi ili kuilinda jamii iweze kuepukana na madhara yatokanayo na matokeo ya matumizi
na upimaji usio sahihi katika Biashara, Afya, Usalama na Mazingira.
Vilevile,
Wakala wa Vipimo husimamia matumizi sahihi ya vipimo kwa njia ya kufanya
ukaguzi wa mara kwa mara (scheduled and surprise inspections), Kukagua bidhaa
zilizofungashwa (prepacked goods) toka nje ya nchi na zile
zinazozalishwa hapa nchini, Kuidhinisha aina mpya ya vipimo vinavyoagizwa toka nje ya nchi na
vinavyoundwa hapa nchini (pattern approval), Kutoa ushauri wa kitaalamu
kuhusiana na vipimo, Kutoa vibali vya Ugezi na leseni za ufundi na uundaji wa
vipimo mbalimbali, Kuiwakilisha nchi Kikanda na Kimataifa katika masuala ya
vipimo.
Meneja
wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Ruvuma ndugu Nyagabona Mkanjabi aliwahasa
wafanyabiashara hao kujiepusha na vitendo vya uchezeaji wa vipimo kwa lengo la
kutaka kujipatia faida zaidi kwani kufanya hivyo ni kinyume cha Sheria ya
Vipimo Sura na. 340 na mapitio yake mbalimbali ambayo inaeleza adhabu kwa mtu
atakaye kutwa amechezea vipimo ni faini isiyopungua shilingi laki moja
(100,000/=) na isiyozidi millioni ishirini (20,000,000/=) kwa kosa. Hivyo, wito
umetolewa kwa watumiaji wote wa vipimo kuzingatia matumizi sahihi ya vipimo na
wafanyabiashara hao wameaswa kutembelea ofisi za wakala wa vipimo zilizopo katika
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kwa ajili ya kupata ushauri wa kitaalamu kuhusu
vipimo au kutoa maoni na kuwasilisha malalamiko yao ili yaweze kufanyiwa kazi
kwa lengo la kuboresha utoaji huduma bora kwa Wananchi.
Pamoja
na hayo wafanyabiashara walielezwa madhara mbalimbali yatokanayo na matumizi
yasiyo sahihi ya vipimo ambayo ni pamoja na kukiuka Sheria ya Vipimo ambayo
inaweza kusababisha mfanyabiashara kuadhibiwa kwa kulipa faini au kupata adhabu
ya kifungo mahakamani na mali yake kutaifishwa. Pia, kumuibia mteja kwa
kumpunja ni moja wapo ya wizi na nikinyume na maandiko ya vitabu vitakatifu,
lakini vilevile biashara zinaweza kufa ama kufirisika kwa kuzidisha bidhaa kwa
wateja pasipo kutumia vipimo vilivyo sahihi katika biashara.
Akizungumza
na mwandishi wetu mshiriki wa mafunzo hayo ndugu Mathew ambaye ni
mfanyabiashara wa gesi songea amewapongeza sana Wakala wa Vipimo kwa kuwapatia
elimu ya matumizi ya vipimo sahihi kwani itawasaidia sana ili kuepuka kujipunja
na kuwapunja wateja wao na kuhakikisha wanatumia mizani mkatika uuzaji na ununuzi
wa bidhaa mbalimbali na amewataka zaoezi ilo liwe endelevu mara kwa mara.