WAKALA WA VIPIMO YASISITIZA MATUMIZI YA VIPIMO SAHIHI CHATO
Imewekwa:August 26, 2021
Wakala wa Vipimo inawakaribisha Wananchi wote wa Chato pamoja na maeneo ya karibu kutembelea katika banda lake kwenye Maonesho ya kUtalii na Biashara yanayofanyika katika Uwanja wa Magufuli Chato. Lengo kuu la Wakala wa Vipimo kushiriki katika maonesho hayo ni kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya Vipimo kwenye sekta mbalimbali.
Meneja
wa Wakala wa Vipimo Bw. Moses Ntungi ameeleza kuwa uwepo wa maonesho haya umesaidia
wananchi wa Wilaya ya Chato kujifunza mambo mbalimbali na kazi zinazofanywa na
taasisi ya Wakala wa Vipimo ikiwa ni pamoja na kutambua umuhimu wa kutumia
vipimo sahihi pamoja na kutambua vipimo vilivyohakikiwa na vile visivyohakikiwa
(batili).
Meneja
Ntungi ameeleza kuwa Vipimo vyote vilivyohakikiwa na Wakala wa Vipimo huwekewa
alama maalumu ambayo ni stika inayosaidia mtumiaji wa kipimo kutambua kwa
urahisi kama kipimo anachotumia kipo sahihi na kimehakikiwa.
Kwa
upande wake Afisa Vipimo Bw. Festo Robert ameeleza kuwa Wakala wa Vipimo katika
Wilaya ya Chato hutekeleza majukumu mbalimbali ili kuwalinda Wananchi. Majukumu
hayo ni pamoja na kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu masuala mbalimbali ya Vipimo,
kufanya uhakiki wa Vituo vyote vinavyouza mafuta, kufanya uhakiki wa bidhaa zilizofungashwa
ili kuhakikisha mnunuzi anapata bidhaa iliyokatika Vipimo sahihi.
Pia,
Bw. Festo ameeleza kuwa Wakala wa Vipimo inafanya uhakiki wa mizani
zinazotumika kuuzia na kununulia zao la pamba ili kuhakikisha kunakuwa na
bishara ya usawa bila kuwa na dhuluma kwa upande wowote. Kadhalika Wakala uhakiki
mizani midogo inayotumika kuuzia bidhaa kwenye maduka na masoko. Vilevile
Uhakiki wa Vipimo hufanyika katika masoko ya madini pamoja na mizani ya kupimia
magari barabarani, na kwenye maghala ya vyama vya msingi vya ushirika.
Kadhalika,
Meneja Ntungi alieleza kuwa Ushiriki wa Wakala wa Vipimo Katika maonesho ya
Kuhamasisha Biashara na Utalii Wilaya ya Chato ni muendelezo wa kuhakikisha
Wananchi katika maeneo mbalimbali wanafikiwa na kupatiwa elimu kuhusu matumizi
sahihi ya Vipimo, lakini pia ushiriki wa Wakala wa Vipimo katika maonesho
mbalimbali husaidia kusikiliza kero za wananchi kuhusu mambo ya vipimo na
kuyatolea ufumbuzi ili kuendelea kuwalinda watumiaji wa vipimo kuweza kupata
huduma bora.
Meneja
Ntungi ametoa onyo kwa Wafanyabiashara kujiepusha na vitendo vya kuchezea
vipimo kwani kufanya hivyo ni kosa na nikinyume na Sheria ya Vipimo Sura na.
340 na mapitio yake ya mwaka 2002. Endapo mfanyabiashara atakamatwa kwa
udanganyifu wa Vipimo na kukiri makosa yake atapigwa faini isiyopungua laki
moja (100,000/=) na isiyozidi milioni 20 endapo atakataa na kufikishwa
mahakamani kwa mkosaji wa kosa la kwanza atatozwa faini isiyopungua laki tatu
(300,000/=) na isiyozidi milioni 50 au kifungo kisichozidi miaka miwili (2) au
vyote kwa pamoja. Pia, endapo mtuhumiwa atakuwa na makosa ya kujirudia atatozwa
faini isiyopungua laki tano (500,000/=) na isiyozidi milioni 100 au kifungo
kisichozidi miaka mitano (5) au vyote kwa pamoja.
Wakala wa Vipimo inawasihi wananchi kutoa taarifa endapo watabaini uchezewaji wa vipimo katika maeneo mbalimbali kupitia namba ya bure 0800 110097 au kutembelea ofisi yeyote ya Wakala wa Vipimo zilizopo katika Mikoa yote Tanzania Bara kwa lengo la kupata ushauri wa masuala ya Vipimo au kuwasilisha malalamiko yao kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wa Wakala wa Vipimo.