WAKALA WA VIPIMO YATOA ELIMU KWA WADAU WA MBOGA MBOGA WILAYANI GAIRO.

Imewekwa:February 16, 2024

Wakala wa Vipimo (WMA) imetoa elimu kuhusu matumizi sahihi Vipimo kwa wasafirishaji, wafanyabiashara, wazalishaji na wakulima wa mboga mboga Wilaya ya Gairo, Mkoani Morogoro.

Kikao hicho cha elimu ya vipimo kilifunguliwa na kusimamiwa na Mkuu wa Wilaya ya Gairo Mhe. Jabir Makame na kuhudhuriwa na Afisa Mtendaji Mkuu Wakala wa Vipimo Bi. Stella Kahwa, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Gairo Bi. Sharifa Yusuph Nabalanga'nya na Katibu Tawala Ndugu. Jeremiah Mapogo.

Mhe. Jabir akifungua kikao hicho aliwaeleza wadau wa mboga mboga kuwa wakala wa vipimo imeitikia wito wa kuja kutoka elimu ya vipimo kama walivyo wasilisha ombi lao mara baada ya mizigo yao kukamatwa ikiwa na uzito zaidi ya ule unao kubalika kisheria.

Vilevile, Mhe. Jabir amewataka wadau wa mboga mboga kufuata kanuni, taratibu na Sheria zilizowekwa ili kuepuka usumbufu unaoweza jitokeza kwani taasisi ya Vipimo inatekeleza Sheria iliyotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza wakati wa elimu kwa wadau wa mboga mboga Bi. Stella Kahwa Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA ameeleza kuwa Sheria ya Vipimo inaelekeza mazao yote kufungashwa kwa uzito usio zidi 100 kg ambapo mboga mboga nyingi zinasafirishwa zikiwa na uzito wa 120 kg jambo ambalo ni kinyume na Sheria ya Vipimo Sura Na. 340.

Bi. Stella amesisitiza kuwa mara baada ya kutoa elimu ya vipimo Kwa wadau wa mboga mboga anatarajia Kuona mboga zinafungashwa Kwa kuzingatia uzito unaotakiwa kisheria usiozidi 100 kg, na kwa wadau watakao kikuka kuzingatia Sheria hatua Kali zitachukuliwa dhidi yao ikiwa ni pamoja na kushtakiwa Mahakamani.

Bw. Amani Peter Ambaye ni Mkulima wa mboga mboga ameipongeza WMA Kwa elimu ya vipimo inayoelekeza mazao zikiwemo mboga mboga kuuzwa kwa mizani jambo ambalo litawasaidia wakulima kupata faida kutoka kwenye mazao wanayo lima.

IMEANDALIWA NA SEHEMU YA MAWASILIANO WMA