WATAALAMU KITENGO CHA BANDARI WMA WAAHIDI WELEDI ZAIDI KAZINI

Imewekwa:August 26, 2024

Na Pendo Magambo – WMA

Wafanyakazi wa Wakala wa Vipimo (WMA) Kitengo cha Bandari, wamesema wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi ili kufikia azma ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwa na Tanzania ya Viwanda. Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi, Meneja anayeongoza Kitengo hicho, Alfred Shungu ameyasema hayo ofisini kwake alipokuwa akizungumza na wanahabari, Agosti 21, 2024.


"Tunatambua kuwa Taifa linatutegemea hususani katika uhakiki wa vipimo na upimaji wa mafuta yanayoingia nchini kuanzia melini, kwenye mita na maghala ya kupokelea mafuta, hivyo tutaendelea kutekeleza majukumu yetu kwa weledi na uadilifu," amesisitiza Shungu.


Akieleza kwa kina kuhusu majukumu ya Kitengo hicho, Shungu amesema msingi wake ni kumlinda mlaji na muuzaji kwa kuhakiki utumiaji wa vipimo sahihi katika biashara ya mafuta hapa nchini. Aidha, amesema, majukumu yao pia yanalenga kuiwezesha serikali kukusanya kodi kwa waagizaji wa mafuta kwa kuhakiki kiasi kilichoagizwa na kampuni zinazoagiza mafuta jamii ya petroli na mafuta ya kula kutoka nje ya nchi.


Shungu amedadavua zaidi kuwa majukumu ya WMA Kitengo cha Bandari katika Meli yanahusisha kuhakiki kiasi cha mafuta yanayowasili nchini kwa kulinganisha na nyaraka za Meli za kuagiza mafuta pamoja na kukagua vipimo vyote vinavyotumika kupimia mafuta. Upande wa Mita, amesema WMA inawajibika kuhakiki mfumo wa upimaji wa mafuta kwa kutumia kipimo kilichohakikiwa na Wakala hiyo. Pia, WMA hupaswa kuweka kumbukumbu ya vipimo na takwimu za matokeo ya upimaji kwa kulinganisha melini na kwenye maghala na kutoa ushauri wa kitaalamu ikibainika kutofautiana.


Aidha, katika maghala, Shungu ameeleza kuwa wajibu wa WMA ni kukagua vipimo vinavyotumika kupima mafuta kwenye matenki, kupima na kuchukua takwimu za kiasi cha mafuta yaliyopo kwenye matenki kabla ya kupokea mzigo pamoja na kuweka alama kwenye matenki yanayopokea mzigo na yasiyopokea mzigo.


Majukumu mengine katika matenki ni kupima na kuchukua takwimu za kiasi cha mafuta yaliyoingia kwenye matenki baada ya kupokea mzigo, saa 24 baada ya mafuta kutulia pamoja na kukokotoa kiasi cha mafuta yaliyoingia katika kila ghala kwa Meli nzima. Amesema baada ya hapo, WMA huandaa taarifa ya upimaji na kusambaza kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) pamoja na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).