WATU WANNE WAKAMATWA KWA KUCHEZEA VIPIMO KWENYE MADUKA YA KUUZIA NYAMA JIJINI DAR ES SALAAM
Imewekwa:March 20, 2023
Wakala wa Vipimo Mkoa wa Dar es Salaam imeendesha ukaguzi wa kushtukiza kwenye maduka ya kuuzia nyama kwa lengo la kujiridhisha kama Vipimo vinatumika kwa usahihi. Takribani maduka 21 yamekaguliwa na Bucha nne zimebainika kufanya udanganyifu kwa kutokutumia Vipimo kwa usahihi ili kuwapunja wanunuzi wa bidhaa hizo.
Akizungumza
mara baada ya zoezi la ukaguzi wa kushtukiza Meneja wa Wakala wa Vipimo Ilala
Bw. Alban Kihulla amesema, kuwa zoezi hilo ni la Kisheria na hufanyika muda
wowote, siku yoyote na saa yoyote lengo likiwa ni kuangalia matumizi ya vipimo
kama yanatumika kwa usahihi kwa mujibu wa Sheria.
Meneja
Kihulla amesema, kwa ukaguzi uliofanyika watuhumiwa wamebainika kuwaibia wateja
wao kiasi cha nusu kilo katika kila kilo mbili zinazonunuliwa na bucha zingine
zimekuwa zikiibia wateja kiasi cha gramu 250 kwenye kila kilo moja ya nyama.
Kihulla
ameeleza kuwa, watuhumiwa wote waliokamatwa wamechukuliwa hatua stahiki kwa
mujibu wa Sheria ya Vipimo Sura ya 340 Mapitio ya 2002 na marekebisho yake ili
iwe funzo kwa wafanyabiashara wengine wenye tabia za kuchezea Vipimo.
Wakala
wa Vipimo inatoa wito kwa Wananchi wote kuwa makini wanapoenda kununua nyama
kwenye maduka mbalimbali na kuwataka washiriki kwenye tukio la upimaji kuliko
kuwa amini wauzaji na endapo watabaini changamoto yoyote wawasiliane nao kwa
namba ya simu ya bila malipo ya 0800 110097 kwa msaada.
Kadharika,
wito umetolewa kwa wauzaji wote wa nyama kuachana na tabia za kuvunja Sheria
kwa kuwaibia wateja wao na wahakikishe wanatenda haki kwa kupima nyama kwa
usahihi na kwenye mizani sahihi iliyohakikiwa kwani kinyume na kufamya hivyo
wataondoa uaminifu kwa wateja wao na watachukuliwa hatua kali za Kisheria.
Vilevile,
wamiliki wa Bucha za nyama wametakiwa kufuatilia mwenendo wa biashara
zinavyofanyika kwenye maeneo yao ya biashara kwa kuwa linapotokea tatizo lolote
la wizi kwa kutotumia mizani kwa usahihi hawatakuwa salama watachukuliwa hatua
kali kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo.