WAZIRI JAFO: WIZI WA KUCHEZEA VIPIMO NI KOSA KISHERIA
Imewekwa:September 19, 2024Na Paulus Oluochi - WMA
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo amehimiza wananchi jijini Mwanza kuzingatia matumizi sahihi ya vipimo kila mara wanapofanya manunuzi na kuuza bidhaa mbalimbali. Aliyasema hayo Septemba 11, 2024 wakati akifungua rasmi Maonesho ya 19 ya Biashara ya Afrika Mashariki yanayofanyika katika Uwanja wa Furahisha jijini Mwanza.
"Wizi wa
kuchezea vipimo ni kosa kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo Sura Na. 340 na hata
vitabu vya dini vinakataza wizi wa vipimo," alisisitiza.
Katika hatua
nyingine, akizungumzia ushiriki wa Wakala wa Vipimo (WMA) katika Maonesho hayo,
Afisa Vipimo Mwandamizi Mkoa wa Mwanza, Lazaro Joram alisema ni mwendelezo wa
utoaji elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya vipimo kwa wafanyabiashara
waliopo ndani ya Mkoa wa Mwanza pamoja na nchi jirani.
"WMA tunatumia
Maonesho haya ili kuwawezesha wadau wetu kutambua majukumu yetu, kueleza
umuhimu wa kuhakiki na kutumia vipimo sahihi na kutoa ushauri wa kitaalamu juu
ya matumizi ya vipimo pamoja na kuendelea kuwaelimisha kuhusu aina za vipimo
vinavyopaswa kutumika katika biashara."
Joram aliwakaribisha
wananchi kutembelea Banda la WMA ili kufahamu aina za mizani wanazoweza kutumia
katika sekta za kilimo, uvuvi, biashara na usafirishaji.
“Tunazo aina nyingi
za mizani lakini siyo kila mzani unaruhusiwa kutumika katika biashara au katika
sekta ya kilimo hivyo ukitembelea Banda letu tutakupa elimu ya kutambua mizani
sahihi iliyohakikiwa pamoja na kutambua alama zinazowekwa katika vipimo vilivyo
hakikiwa,” alisema.
Akidadavua kuhusu
elimu inayotolewa kwa wananchi wanaotembelea Banda la WMA, Joram alisema eneo
mojawapo ni kuhusu namna sahihi ya ufungashaji wa mazao ya shamba ambapo kwa
mujibu wa Sheria ya Vipimo mazao yote yanatakiwa kufungashwa kwa uzito usiozidi
kilogramu mia moja (100 kg) na endapo mkulima atafungasha mazao kwa uzito zaidi
ya uliotajwa kisheria atakuwa amefungasha Lumbesa na hatua kali za kisheria
zitachukuliwa dhidi yake.
“Kwa sasa tafsiri
ya lumbesa ni uzito unaozidi kilo mia moja (100 kg) tofauti na awali ambapo
ilikuwa inatafsiriwa kama kuongeza kifungashio juu ya gunia hivyo tunawahimiza
wakulima kutumia mizani ili kujua uzito wa mazao wanayofungasha,” alisisitiza.
Akieleza zaidi, alisema
kuwa, Kanda ya Ziwa kuna mazao ya kimkakati aina mbili ambayo ni Pamba na
Kahawa ambapo jukumu la WMA ni kuhakiki mizani zote zinazotarajiwa kutumika
kwenye ununuzi wa mazao hayo kabla ya msimu kuanza na baada ya kufanya uhakiki
mizani iliyo sahihi huruhusiwa kutumika katika ununuzi wa mazao hayo.
Vilevile, alisema wakati wa ununuzi, WMA hufanya kaguzi za kushtukiza katika Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS) ili kujiridhisha kama mizani zinatumika kwa usahihi kama zilivyo hakikiwa ili kuwalinda wakulima. Pamoja na majukumu mengine, WMA pia ina jukumu la kusimamia usahihi wa vipimo kwenye sekta ya usafirishaji ambao ni pamoja na usafiri wa anga, barabara na usafiri wa majini kwa kuhakikisha mizani zinazotumika ziko sahihi na zimehakikiwa ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza ikiwemo kubeba mizigo yenye uzito mkubwa ambayo inaweza kusababisha vyombo hivyo kuanguka na miundombinu kuharibika.
Kwa upande wake,
Afisa Uhusiano Mwandamizi wa WMA anayeshiriki Maonesho hayo, Paulus Oluochi alitoa
wito kwa wananchi kutembelea Banda la WMA ili kujifunza kuhusu matumizi sahihi
ya vipimo lakini pia kuwasilisha changamoto mbalimbali kama zipo ili ziweze
kupatiwa ufumbuzi.
Alisema endapo
mwananchi yupo mbali, anaweza kuwasiliana na WMA kupitia nambari isiyo na
malipo 0800 110097.
Maonesho
hayo ya 19 ya Biashara ya Afrika Mashariki yanatarajiwa kufikia tamati Septemba
15, 2024.