WAZIRI MKUU AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA OFISI YA MAKAO MAKUU YA WAKALA WA VIPIMO (WMA)

Imewekwa:February 09, 2024

Na Mahamudu Jamal

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) ameweka jiwe la msingi katika ujenzi wa ofisi ya Makao Makuu ya wakala wa vipimo (WMA) jijini Dodoma.

Akiongoza ujumbe uliohudhuria katika hafla hiyo ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa ofisi ya wakala wa vipimo (WMA), Mhe. Majaliwa amepongeza wakala wa vipimo kwa hatua kubwa iliyofikia katika ujenzi wa ofisi yake eneo la Medeli jijini Dodoma kwa kutumia mapato yake ya ndani huku akisisitiza kuzingatia ubora katika ujenzi na kukamilisha kwa wakati na kuanza kazi iliyokusudiwa.

Aidha, Mhe. Majaliwa amepongeza hatua ya Wakala wa vipimo (WMA) kutumia mkandarasi mzawa katika ujenzi wa jengo la ofisi ya makao makuu ya taasisi hiyo na kusisitiza taasisi za Serikali kutumia wakandarasi wazawa wenye uwezo na vigezo vya kupewa zabuni hizo.

Mhe. Majaliwa ameongeza kuwa ujenzi wa ofisi za Serikali jijini Dodoma ni hatua nzuri ya kuendelea kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuboresha mazingira ya ufanyaji kazi kwa watumishi na kusogeza huduma muhimu kwa wananchi.

Mhe. Majaliwa amewataka Wakala wa Vipimo (WMA) kuhakikisha inamlinda mlaji kwa kuhakiki na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa vipimo, bidhaa na huduma mbali mbali zitolewazo nchini na kuwataka Wafanyabiashara wote kufanya biashara kwa kuzingatia vipimo sahihi ili kukuza uchumi wa Tanzania.

Sanjari na hayo, Mhe. Kassim Majaliwa amesisitiza Wakala wa Vipimo juu ya upimaji wa mita za maji, umeme na vipimo vyote vinavyohusika na utoaji wa huduma kwa mlaji na kuwataka WMA kushirikiana na kusomana vyema na taasisi zote za Serikali na binafsi zinazotumia vipimo katika utendaji wake ili kupunguza na kuondoa migogoro na kuleta matokeo chanya kwa uchumi wa taifa.

Katika hatua nyingine Mhe. Kassim Majaliwa amepokea vyema ombi la wakala wa vipimo (WMA) lililo wasilishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Vipimo Tanzania Dkt. Elizabeth Mwakasangula la kufanya Wakala wa Vipimo kuwa Mamlaka kamili ili kuleta tija na ufanisi katika utendaji wake.

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) amemshukuru Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa kutambua kwa dhati umuhimu na kazi kubwa ya wakala wa vipimo katika kumlinda mlaji na kuchochea ukuaji wa uchumi na ustawi chanya wa taifa.

Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuwa ujenzi wa jengo la ofisi ya wakala wa vipimo unatekelezwa kwa mapato ya ndani huku ujenzi huo ukigharimu shilingi bilioni 6.170 na kutarajia kukamilika januari 2025.

Dkt. Ashatu ameongeza kuwa kukamilka kwa jengo hilo kutasaidia kuboresha huduma zitolewazo na taasisi hii kutokana na uwepo wa miundo mbinu na vitendea kazi bora na vya kisasa.

Aidha, Dkt. Ashatu Kijaji amehitimisha kwa kusema kuwa ujenzi wa jengo la ofisi ya Makao Makuu ya Wakala wa Vipimo utakwenda sambamba na ujenzi na uboreshaji wa ofisi za mikoa ili kusogeza huduma karibu na Wananchi.

Katika taarifa yake muhimu aliyo wasilisha mbele ya Mgeni Rasmi, Afisa mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo Bi. Stella Kahwa ametanabaisha kuwa, Wakala wa Vipimo ilikuwa na mkakati wake wa kujenga jengo la ofisi ya makao makuu jijini Dodoma, kwa kuzingatia mpango mkakati wa WMA wa mwaka 2021-2022 na 2025-2026.

Bi.Stella Kahwa ameongeza kuwa, Wakala wa Vipimo ilipata msukumo chanya wa Serikali na hivyo kuanza mchakato wa ujenzi wa jengo hilo ambapo WMA ilipata kiwanja nambari 136,kitalu AC chenye ukubwa wa mita za mraba 2742 katika eneo la Medeli.

“Mradi huu ulianza na usanifu wa majengo, kazi uliyofanywa na kitengo cha ushauri wa kitaalamu kutoka Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST) ,baada ya hapo wakala wa vipimo aliingia mkataba na kampuni ya wazawa ya ujenzi ya Mohammed Builders, kwa makubaliano ya malipo ya shilingi bilioni 6.170 ambapo hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 70% na mkandarasi ameshalipwa shilingi bilioni 3.254. Jengo hili litakuwa la ghorofa tano, litakuwa na jumla ya vyumba vya ofisi stini, maabara ya kisasa moja, ukumbi mkubwa wenye uwezo wa kuhudumia watu mia moja, ukumbi mdogo wenye uwezo wa kuhudumia watu ishirini, maktaba ndogo moja, kantini moja na eneo la maegesho ya magari lenye uwezo wa kuhudumia magari arobaini na moja. Ujenzi wa jengo hili ulianza julai 02 mwaka 2022 na unatarajia kukamilika januari mwaka 2025” alisema Bi.Stella Kahwa.

Wakala wa Vipimo (WMA) imekuwa taasisi ya kwanza katika Wizara ya Viwanda na Baishara kuanza mchakato wa ujenzi wa ofisi za Makao Makuu yake jijini Dodoma kwa kutumia fedha zinazotokana na mapato ya ndani, huku ujenzi huo ukielekea kukamilika katika muda elekezi.

Sanjari na hayo WMA kupitia mpango mkakati wake, inatarajia kuanza mchakato wa haraka wa ujenzi wa ofisi zake katika mikoa ya Songwe, Lindi na Ruvuma lakini pia, ukarabati mkubwa wa ofisi ya WMA ilala na hivyo kuhuisha na kusogeza huduma bora kwa Wananchi.