WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA ATEMBELEA KITUO CHA UHAKIKI WA VIPIMO MISUGUSUGU

Imewekwa:July 11, 2024

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Selemani Jafo (Mb) ametembelea kituo cha uhakiki wa vipimo misugusugu mkoani Pwani na kupokelewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA) ndugu. Alban Mark Kihulla.

Akiongoza ujumbe kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, waziri Dkt. Jafo ametembelea jengo linalofanya uhakiki wa dira za maji, jengo la kuhakiki mita za umeme, pamoja na sehemu ya kufanyia uhakiki wa matenki ya magari yanayotumika kusafirishia vimiminika ndani na nje nchi.

Katika ziara hiyo, waziri Dkt. Jafo ameshuhudia utendaji kazi wa mitambo mbalimbali ya uhakiki wa dira za maji na mita za umeme unaofanywa na Wakala wa Vipimo katika kituo hicho cha uhakiki wa vipimo misugusugu.

Aidha, Waziri Dkt. Jafo amepokea maelezo kutoka kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo ndugu Alban Kihulla juu ya utendaji kazi wa WMA katika maeneo mbalimbali na takwimu jumuishi za miaka mitatu (2022 -2024) ya utendaji kazi wa WMA.

“Mheshimiwa Waziri, Dkt. Selemani Jafo karibu sana katika kituo chetu cha uhakiki wa vipimo kilichopo hapa misugusugu mkoani Pwani, kituo hiki ni maalum kwa uhakiki wa dira za maji, mita za umeme na Magari yanayotumika kusafirisha vimiminika. Katika kituo hiki tuna mitambo mikubwa miwili ya uhakiki wa mita za umeme na kila mtambo unahakiki mita 20 kwa mara moja ambapo kwa siku tunahakiki mita 1200 za umeme, lakini pia tuna mtambo mwingine wa kuhakiki mita za umeme uliopo mkoani Kilimanjaro. Mhe.Waziri hadi sasa tumekwisha hakiki mita 4500 kutokana na mitambo hii ya kisasa tuliyonayo” alisema ndugu Kihulla akimueleza Waziri, Dkt. Jafo.

Ndugu Kihulla ameongeza kuwa, WMA inafanya uhakiki wa mita za umeme na dira za maji kwa ufanisi mkubwa lengo likiwa ni kusimamia haki na kuleta usawa katika biashara baina ya mtoa huduma na mteja na kuepusha madhara yatokanayo na matumizi yasiyo sahihi ya vipimo.

Ndugu Kihulla amemueleza Mhe.Waziri Dkt. Jafo kuwa Wakala wa Vipimo inaendelea kujikita katika utoaji wa huduma bora na zenye ufanisi kwa kuwafikia wananchi kwa upana wake kutokana na kuwepo kwa ofisi za Wakala wa Vipimo katika mikoa yote ya Tanzania bara, lakini pia uwepo wa ofisi za WMA katika mipaka yote ya nchi kama namanga,holili,sirari,tarakea na tunduma ambapo bidhaa zinazoingia kupitia mipakani uhakikiwa kabla haijaingia nchini.

Aidha, ndugu Kihulla ameongeza kuwa, WMA inaendelea kutekeleza majukumu yake muhimu na ya kimkakati kwa kujiwekea malengo na kuyafikia malengo hayo kwa wakati unaotakiwa.

Ndugu Kihulla amesema kuwa “ katika miaka mitatu iliyopita, mwaka wa fedha 2021-2022 Wakala wa Vipimo ilifikia lengo na hata kuvuka kwa asilimia moja katika ukusanyaji wa ada na mapato yanayotokana na utekelezaji wa majukumu ya msingi ya WMA, mwaka wa fedha 2022-2023 WMA imefikia malengo yake kwa asilimia 98 na mwaka wa fedha 2023-202 wakala imefikia malengo kwa asilimia 83.5. Katika mwaka wa fedha uliopita (2023-2024), WMA ilifanikiwa kukusanya mapato kiasi cha shilingi Bilioni 31.616 ya mapato yatokanayo na ada mbalimbali zinazokusanywa na wakala, mapato hayo ni asilimia 99.6 ya ufikiwaji wa malengo ya WMA katika mwaka huo wa fedha.Lakini pia WMA imepanga kukusanya Bilioni 39.65 katika mwaka huu mpya wa fedha”

“Tutaendelea kuangalia fursa mbambali za ukuaji katika muktadha wa vipimo, tutaendelea kuchangia katika mfuko wa Serikali kwa wakati, na kwa bahati nzuri Mheshimiwa Waziri sisi WMA tumeshinda tuzo hivi karibuni ya taasisi inayotoa gawio kwa serikali kwa wakati, tuzo hii tulikabidhiwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Tumejipanga kufanya kazi kwa bidii na kufikia malengo yetu.” Alisema ndugu Kihulla.

Sanjari na hayo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo,ndugu Alban Kihulla amemueleza Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Seleman Jafo changamoto mbalimbali za WMA ikiwemo upungufu wa watumishi katika taasisi hiyo ambapo ina watumishi 270 kati ya 581 wanaotakiwa na taasisi hiyo na hivyo kuwepo na upungufu wa watumishi 311.

Aidha, Ndugu Kihulla ametanabaisha malengo ya WMA kwa mwaka huu wa fedha kuwa ni kununua vifaa na mitambo mipya na ya kisasa ili kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia na ukuaji wa biashara kwa ujumla, kuwajengea uwezo na uzoefu mkubwa watumishi wa WMA katika nyanja mbalimbali ili kutoa huduma bora na kwa ufanisi mkubwa kwa wananchi, lakini pia kujiimarisha katika mifumo yake na kuongeza ufanisi katika kusomana kwa mifumo na wakuu wa taasisi zingine za serikali katika utoaji wa huduma.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Vipimo Profesa Eliza Mwakasangula amemshukuru Waziri, Mhe. Dkt. Jafo na ujumbe wake kwa kuitembelea Wakala wa Vipimo na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na taasisi hiyo katika kuwahudumia wananchi.

Profesa Eliza Mwakasangula amemuomba Waziri Mhe, Dkt. Jafo kusimamia mchakato wa kuifanya WMA kuwa Mamlaka ili kutanua wigo na ufanisi katika utendaji kazi wake na kuwahudumia wananchi sanjari na kuchochea maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt, Seleman Jafo amemshukuru Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo ndugu Alban Kihulla na watumishi wa wakala kwa kumpokea vyema na kumpitisha katika maeneo mbalimbali ya kiutendaji.

“Leo nimekuja kuwatembelea ndugu zangu wa Wakala wa Vipimo katika kituo chenu cha uhakiki wa vipimo cha misugusugu kwa lengo kufahamiana na ninyi kwanza, lakini pia mmenipitisha kwenye maeneo ya utendaji kazi, mnafanya kazi nzuri na ninawapongeza sana”

“mimi ni mtu wa kazi kwa hiyo Afisa Mtendaji Mkuu naomba sasa mjipange vyema kwa sababu kazi ndo imeanza na tukutane eneo la kazi (site)” amesema Mhe. Jafo.

Katika hatua nyingine Mhe. Dkt Jafo amemuagiza Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA kuhakikisha mita zote za umeme na dira za maji zinahakikiwa na WMA na kupelekwa kwa wananchi katika muda muafaka bila ya kuwepo na kikwazo chochote.

“Nakuagiza ndugu Afisa Mtendaji Mkuu, hakikisha mita zote za umeme na maji zinahakikiwa hapa bila ya kikwazo chochote, ofisi yangu iko wazi muda wote leteni kanuni zozote zitakazofanya zoezi la uhakiki kufanikiwa kwa asilimia zote. Lakini pia hakikisha unakaa na taasisi zingine kama TANESCO na zingine mjue namna bora ya kufanya kazi katika hilo, baada ya muda nitahitaji ripoti ya hatua mliyofikia” alisema Mhe. Jafo.

Aidha Mhe. Jafo amemuelekeza Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo kuelekeza nguvu zake katika mapambano dhidi ya ufungashaji holela wa mazao ( lumbesa), ufungasshwaji wa saruji, nondo na mabati ili kupambana na wafanyabiashara na wazalishaji wote wenye nia ovu ya kuchezea vipimo kwa manufaa yao binafsi.

Waziri Mhe. Dkt. Jafo ameitembelea WMA ikiwa ni taasisi ya pili kuitembelea kati ya taasisi 13 zinazounda Wizara ya Viwanda ya Biashara tangu kuteuliwa kwake kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara huku akisisitiza utendaji kazi bora na wenye tija kwa maendeleo y