WMA ILALA YATEKELEZA MKAKATI WA ELIMU MASOKONI KWA KILA MDAU
Imewekwa:June 25, 2024
WAKALA WA VIPIMO MKOA WA ILALA YATEKELEZA MKAKATI WA ELIMU MASOKONI KWA KILA MDAU
Wakala
wa Vipimo Mkoa wa Ilala imetekeleza mpango mkakati wake wa utoaji wa elimu juu
ya matumizi sahihi ya vipimo na ufungashaji wa mazao kwa usahihi kwa mujibu wa
Sheria ya Vipimo.
Zoezi
hilo la utoaji wa elimu, limefanyika katika soko la Ilala ambapo maafisa vipimo
kwa kushirikiana na viongozi wa soko wamepita katika kila ghala, kitalu na
maeneo yote ya biashara sokoni hapo na kutoa elimu ya matumizi sahihi ya vipimo
na kuwajengea ufahamu juu ya Sheria mbalimbali za Vipimo.
Zoezi
hilo la utoaji elimu kwa wadau na wafanyabiashara masokoni ni endelevu ambapo
Maafisa Vipimo wa Mkoa wa kivipimo wa Ilala watapita katika kitalu, ghala na
sehemu mbalimbali za biashara na kutoa elimu ya matumizi sahihi ya vipimo kwa
kila mdau na mfanyabiashara.
Aidha,
Meneja wa Mkoa wa Kivipimo wa Ilala Bw.Muhono Nashon amekutana na kufanya kikao
na viongozi wa kamati ya soko la buguruni katika ofisi za Wakala wa Vipimo Mkoa
wa Ilala.
Katika
kikao hicho, Bw. Nashon amewaasa Viongozi hao wa soko la Buguruni kuwafikishia
ujumbe wafanyabiashara kutoka Wakala wa Vipimo juu ya matumizi sahihi ya vipimo
na kuwa mabalozi wazuri katika maeneo yao ya biashara.
Sanjari
na hayo, Bw. Nashon ameweka mikakati ya ushirikiano chanya baina ya viongozi
hao na WMA katika kutokomeza ufungashaji holela wa mazao (lumbesa) na udhibiti
wa matumizi yasiyo sahihi ya vipimo katika maeneo mbalimbali ya biashara kama
matumizi ya makopo na visado.
Huku
hayo yakijiri, Bw. Nashon ameendelea na mapambano dhidi ya ufungashaji holela
wa mazao (lumbesa) ambapo amefanikiwa kukamata na kuliweka kizuizini gari lenye
namba za usajili T790 DLC kwa kosa la kupakia mazao yaliyofungashwa katika
uzito wa zaidi ya kilogramu 100 (lumbesa) na kukiuka Sheria ya Vipimo.
Bw.
Nashon amesema kuwa ukamataji huo umetokana na kaguzi za kushitukiza
zinazofanywa na WMA katika nyakati mbalimbali kwa kupita katika maghala, vitalu
na njia za usafirishaji ili kubaini ufungashaji wa mazao hayo.
Bw.Nashon ameongeza kuwa mmiliki wa gari hilo na wahusika wote katika ufungashaji huo holela (lumbesa) watachukuliwa hatua za kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo.