WMA YAKAGUA MIZANI INAYOTUMIKA KATIKA SEKTA YA MADINI

Imewekwa:September 30, 2023

Wakala wa Vipimo (WMA) inawakaribisha wananchi wote wa Geita na Mikoa yote ya karibu kuhudhuria katika maonesho ya sita ya Kimataifa ya Madini ambayo yanafanyika katika viwanja vya EPZA bombambili mwatulole. Lengo kubwa la Wakala wa Vipimo kushiriki katika maonesho haya ni kuwapa elimu Wananchi na wadau wa sekta ya madini kuhusu matumizi sahihi ya vipimo pamoja na kuwaelezea majukumu ya Wakala wa Vipimo katika sekta mbalimbali hususani ya Madini.

Wakala wa vipimo inaishukuru sana serikali ya awamu ya sita ambayo inaongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kusimamia sekta ya madini ambapo kwa mkoa wa geita kuna jumla ya masoko kumi (10) ya kuuzia na kununulia dhahabu ambayo ni Geita mjini, Katoro, Chato, Lwamgasa, Nyarugusu, Mbogwe, Bukombe, Nyang’wale, Mgusu na Nyakagwe.

Akizungumza na mwandishi wetu Kaimu Meneja Wakala wa Vipimo Geita Bi. Eva Ikula amesema kuwa, Wakala wa Vipimo inamchango mkubwa katika sekta ya madini ambapo biashara hiyo haiwezi kufanyika bila kuwa na mizani sahihi na iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo ili kuweza kutambua uzito halisi wa dhahabu inayonunuliwa au kuuzwa. Jukumu kuu la Wakala wa Vipimo katika sekta hii ni kuhakikisha mizani yote inayotumika kuuzia na kununulia vito na madini inahakikiwa na inapima madini kwa usahihi na pia taasisi hiyo inahakikisha inatoa ushauri wa kitaalamu juu ya mizani zinazopaswa kutumika kuuzia madini kwa kuwa siyo mizani yote inastahili kutumika kuuzia na kununulia madini.

Pia, ameeleza kuwa mara baada ya uhakiki wa mizani hiyo kukamilika uwekewa alama maalumu ambayo inaonesha utambuzi kuwa mizani imehakikiwa na inafaa kutumika kununulia madini. Alama zinazowekwa katika mizani iliyohakikiwa ni stika pamoja na lakiri (seal) ambayo inakuwa na alama ya nembo ya taifa pamoja na tarakimu mbili za mwisho za mwaka husika mfano (23) ikiashiria imehakikiwa 2023.

Vilevile, Meneja Eva ameeleza kuwa lengo na dhumuni la Wakala wa Vipimo kufanya uhakiki wa mizani ya kuuzia na kununulia madini ni kuhakikisha matumizi ya mizani sahihi iliyohakikiwa yanazingatiwa na kunakuwa na biashara ya usawa ambapo itawezesha Serikali kukusanya mapato kwa usahihi na wauzaji wa madini wanapata fedha stahiki kulingana na thamani ya madini wanayouza. Kadhalika, mara baada ya uhakiki wa mizani inayotumika kuuza na kununulia madini Wakala wa Vipimo hufanya kaguzi za kushtukiza mara kwa mara katika masoko ya kuuzia madini ili kujiridhisha kama mizani bado ipo sahihi na inatumika kwa usahihi kama inavyostahili.

Ngugu Patrick Charles ambaye ni mfanyabiashara wa soko kuu la dhahabu geita amesema wakala wa vipimo hupita mara kwa mara kukagua mizani wanayotumia ili kuhakikisha haki inapatikana baina ya muuzaji na mnunuzi wa madini.

Patrick Ametoa wito kwa wafanyabiashara wengine kwenye soko hilo kuhakikisha mizani yao imekaguliwa na ameahidi kuwa balozi kwa wafanyabiashara wengine kwa kuwahimiza kutumia vipimo sahihi wakati wote na kuzingatia matakwa ya Sheria ya Vipimo.

Pia, wananchi wanakaribishwa kutumia namba ya simu ya bure ambayo ni 0800 11 00 97 endapo watakumbana na changamoto yeyote ya kivipimo na kitaalamu ili iweze kufanyiwa kazi kwa wakati au wafike kwenye ofisi ya wakala wa vipimo Geita iliyopo eneo la Bomani.