WMA YAPANGA KUNG'ARA SHIMUTA
Imewekwa:September 02, 2024Ikiwa imebaki miezi miwili kuelekea mashindano ya Shirikisho la Michezo la Mashirika ya
Umma,Taasisi na Makampuni Binafsi ( SHIMUTA) ambayo yamepangwa kufanyika katika
Viwanja vya CCM Mkwakwani mkoani Tanga kuanzia tarehe 10 hadi 24 Novemba,2024,
Wakala wa Vipimo (WMA)imefanya bonanza la michezo leo Agosti 31,2024, katika viwanja
vya Tcc Chang'ombe (Gwambina) Jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya
Mashindano hayo.
Katika kuhakikisha kuwa WMA inapata timu bora na yenye ushindani, Watumishi wa Taasisi
hiyo wameshriki michezo katika bonanza hilo ikiwemo mpira wa miguu,mpira wa pete, drafti, na
kuvuta kamba ili kujiweka tayari na kuwa na utimamu wa mwili kuelekea SHIMUTA.
Akizungumza wakati wa bonanza hilo, Kaimu Mkurugenzi Huduma za Biashara wa WMA Bw.
Karim Mkorehe ameeleza kuwa mazoezi ya kutafuta wachezaji wa kushiriki katika michuano ya
SHIMUTA yameanza mapema ili kuhakikisha ushiriki wa taasisi unakuwa na tija.
Aidha, Mkorehe amesisitiza kuwa ufanyaji wa mazoezi ya pamoja huimarisha afya, na huleta
umoja na hivyo kuwataka watumishi kujenga tabia ya kufanya mazoezi na kujenga utimamu wa
mwili.
"Michezo ni afya na katika siku hii maalumu ya bonanza licha ya kucheza michezo mbalimbali
pia watumishi wamepata nafasi ya kupima afya zao, pia wamepata chanjo ya homa ya ini na
upimaji wa VVU". amesema Mkorehe.
"Leo ni siku ya kwanza ya mazoezi yetu, tutakaa na kuandaa mpango mzuri wa mazoezi ya
mara, tunatarajia kuongeza michezo mingine kama vile kukimbia mbio ndefu na fupi, lengo letu
ni tuwe tayari kwa mashindano ya SHIMUTA na tufanye vizuri". ameongeza Bw.Mkorehe.
Kwa upande wake Mwandishi Mwendesha Ofisi wa WMA Bi. Hamida Salum ameupongeza
Uongozi wa WMA kwa kuona umuhimu wa mazoezi kwa watumishi wake na kutoa wito kwa
watumishi wote wa WMA kujitokeza kwa wingi na kushiriki mazoezi kwa mujibu wa ratiba
husika.
"Leo tumejumuika watumishi wa WMA kutoka ofisi za makao makuu, Ilala,Temeke,Kinondoni
na wenzetu wa mkoani Pwani katika bonanza hili, tumecheza tumefurahi na kuweka miili sawa,
tukiwa na nia na kufanya vizuri mazoezini tutaiwakilisha vyema WMA katika SHIMUTA ya
mwaka huu hapo Tanga". ameongeza Bi Hamida.
Mashindano haya ya SHIMUTA yalianzishwa mnamo mwaka 1967 na kusajiliwa rasmi mwaka
1973. Mashindano hayo hufanyika kila mwaka na huandaliwa kwa awamu na mikoa tofauti
ambayo hupewa dhamana ya kuandaa mashindano kutoka kwa waratibu SHIMUTA. WMA
itashiriki mashindano hayo kikamilifu.