WMA YASISITIZA MATUMIZI SAHIHI YA VIPIMO KWA WAFANYABIASHARA WA MVINYO

Imewekwa:December 03, 2024

Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Dodoma imewahimiza wajasiriamali na wafanyabiashara wanaouza mvinyo unaotokana na zao la zabibu kufungasha bidhaa zao kwa kuzingatia vipimo sahihi ili kutowapunja wateja wao kwa kuhakikisha wanapata ujazo ulio sahihi kulingana na thamani ya fedha wanayotoa kununua bidhaa hizo.

Wito huo umetolewa na Meneja wa WMA Mkoa wa Dodoma Bw. Karim Zuberi alipowatembelea wauzaji wa wine wanaoshiriki katika Tamasha la Dodoma Zabibu Tourism Innternational Fair kwenye Viwanja vya Reli Dodoma Mjini ambapo WMA pia inashiriki kutoa elimu kuhusu matimizi sahihi ya vipimo katika tamasha hilo.

“Zao la zabibu ni moja ya zao la kimkakati ambalo linalimwa sana katika Mkoa wa Dodoma na kupitia zao hilo wafanyabiashara wengi na wajasiriamali huliongezea thamani kwa kutengeneza mvinyo (wine) ambayo hufungashwa kwa kutumia madumu na chupa za ujazo tofauti tofauti, hivyo kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo Sura Na. 340 wanatakiwa kutumia vipimo wakati wa ufungashaji na kuandika ujazo wa vinywaji hivyo kwenye vifungashio ili kumrahisihia mteja kujua ananunua mvinyo wenye ujazo wa kiasi gani.”

Kadharika, Meneja Zuberi anawakaribisha wananchi wa Mkoa wa Dodoma kutembelea banda la WMA katika maonesho hayo ili kuendelea kujifunza juu ya huduma zinazotolewa na Wakala wa Vipimo ikiwa ni pamoja na eneo la uhakiki wa dira za maji mpya pamoja na zile ambazo zipo kwenye matumizi ambazo hufanyiwa ukakiki kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma za maji kupitia vipimo ambavyo vipo sahihi.

Akizungumza na mwandishi wetu Bi. Zaituni Ramadhani mjasiriamali wa mvinyo (wine) zinazotokana na zao la zabibu ameishukulu WMA kwa kutembelea bidhaa zake na kumpa ushauri wa kitaalamu wa namna ya kuboresha ufungasaji wa bidhaa zake ikiwa ni pamoja na kuweka taarifa za eneo ambalo biashara yake inafanyika, mawasiliano pamoja na ujazo wa wine anazofungasha ili mumlahisishia mteja kujua ujazo wa wine anayonunua.

Wakala wa Vipimo inaendelea kutoa wito kwa wafanyabiashara wote kuhakikisha wanatumia vipimo sahihi katika maeneo yao ya biashara kwakuwa kupunja ni kosa kwa mujibu wa sheria na hata vitabu vya dini vinazuia upunjaji kwa kuwaibia wateja.

Meneja Zuberi ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa katika ofisi za WMA zilizopo karibu endapo wanapata changamoto yoyote ya kivipimo au kutoa taarifa kwa namba ya bila malipo 0800 110097 ili kuweza kupata msaada na kukomesha vitendo vya ukiukwaji wa sheria.