WMA YATOA MSAADA WA VIFAA VYA TEHAMA KWA JESHI LA POLISI ILALA
Imewekwa:September 11, 2024Na
Mahamudu Jamal, WMA
Wakala wa Vipimo (WMA) imekabidhi
msaada wa vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa Jeshi la
Polisi Mkoa wa kipolisi Ilala, Septemba 10, 2024 katika hafla iliyofanyika
Makao Makuu ya Jeshi hilo Jijini Dar es Salaam.
Akiongoza makabidhiano hayo kwa niaba
ya Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Meneja wa Mkoa wa kivipimo Ilala Muhono Nashon
alisema msaada huo ni kutokana na ushirikiano wa muda mrefu katika masuala ya
kazi baina ya WMA na Jeshi la Polisi hususani katika masuala ya jinai, ulinzi
na usalama kwa maeneo mbalimbali ya ukaguzi, na nyanja nyinginezo.
Meneja Muhono amebainisha kuwa
ushirikiano huo baina ya WMA na Jeshi la Polisi umekuwa na tija kutokana na Jeshi hilo kudumisha hali ya amani na usalama
kwa watumishi wa WMA na wananchi kwa ujumla katika shughuli mbalimbali za
kimaendeleo.
Aidha, ameongeza kuwa, WMA imekabidhi
vifaa hivyo ili kuunga mkono matumizi ya TEHAMA kwa taasisi mbalimbali za Serikali
ikiwemo Jeshi la Polisi.
“Vifaa hivi vitatumiwa na Jeshi letu
katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali na ni matumaini yetu kuwa vitaongeza
ufanisi katika utendaji wake,” amesema Nashon.
Kwa Upande wake Kamishna Msaidizi wa
Polisi na Afisa Mnadhimu wa Mkoa wa Kipolisi Ilala Mohammed Makusi, ameishukuru
WMA kwa msaada huo na kusisitiza kuwa Jeshi hilo litaendelea kutumia TEHAMA
katika utekelezaji wa majukumu yake ili kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi.
“Vifaa hivi vimekuja wakati muafaka,
tukielekea katika Wiki ya Maadhimisho ya Miaka 60 ya Jeshi la Polisi Tanzania
ambayo yatafikia kilele chake tarehe 27, Septemba, 2024”
Alisema kuwa, Kauli Mbiu ya Maadhimisho
hayo kwa mwaka huu ni Huduma bora za kipolisi zitapatikana kwa kubadili fikra, usimamizi
wa sheria na matumizi ya TEHAMA.
“WMA mmetuunga mkono katika TEHAMA,
hivyo tunawashukuru kwa hiki mlichotupatia ambacho kitasaidia kuboresha huduma
zetu,” amesisitiza Kamishna Msaidizi Makusi.
WMA imekuwa na utaratibu endelevu wa kuimarisha ushirikiano na wadau pamoja na Taasisi mbalimbali za Serikali na Binafsi kwa kutoa elimu ya matumizi sahihi ya Vipimo, ushauri wa kitaalamu, semina elekezi na uwezeshaji kwa baadhi ya Taasisi.