Maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani

Imewekwa:May 19, 2021

Kila mwaka Mei 20, Wakala wa Vipimo (WMA) huungana na mashirika mengine ulimwenguni kuadhimisha Siku ya Vipimo Duniani. Wakala wa Vipimo ni mwanachama wa Shirika la Vipimo Duniani (OIML) na kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu 2021 ni Vipimo katika sekta ya Afya (Measurements in health).

katika kuadhimisha siku hii Wakala wa Vipimo imefanya mfululizo wa kuhakiki mizani zote zinazotumika katika hosptitali mbali mbali na vituo vya afya katika Mikoa yote Tanzania Bara ili kujiridhisha kama mizani hiyo inapima kwa usahihi kwa lengo la kuwalinda wagonjwa wanaofika katika vituo hivyo kupata huduma. Wakala wa Vipimo inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo Sura Na. 340 na mapitio yake mbalimbali. Hivyo, kwa mujibu wa Sheria Wakala wa Vipimo uhakiki vipimo vyote ikiwa ni pamoja na mizani zitumikazo katika hospitali mbalimbali ambapo kwa mwaka ukaguzi hufanyika mara moja na baadae hufanyika ukaguzi wa kushtukiza ili kujiridhisha kama vipimo hivyo vinatumika kwa usahihi.

Endapo mizani hubainika kuwa na itilafu Wakala wa Vipimo hukataa kuipitisha na kuelekeza kupelekwa kwa mafundi mizani ili kuifanyia matengenezo na mara baada ya fundi kurekebisha maafisa wa Wakala wa Vipimo hupita kuihakiki na ikikidhi vigezo huruhusiwa kutumika na kuwekewa stika maalumu ya ukaguzi ya Wakala wa Vipimo.

Uhakiki wa Mizani katika sekta ya afya husaidia wagonjwa kupatiwa matibabu kwa usahihi kulingana na uzito mgonjwa alionao, kinyume na kufanya hivyo kunaweza kusababisha mgonjwa kupatiwa dozi kubwa ya dawa ambayo haiendani na uzito wake hivyo kusababisha madhara makubwa katika afya ya mgonjwa husika.

"Zingatia matumizi sahihi ya Vipimo kukuza uchumi wa nchi"

"Zingatia matumizi sahihi ya Vipimo kuokoa nguvu kazi ya Taifa"