YALIYOJIRI KATIKA HAFLA YA KUWAPONGEZA WANAFUNZI WALIOFANYA VIZURI ZAIDI CHUO CHA CBE DAR ES SALAAM

Imewekwa:November 10, 2023

Afisa Mtendaji Mkuu Wakala wa Vipimo Bi. Stella Kahwa leo tarehe 9/11/2023 alikuwa Mgeni Rasmi katika hafla ya kuwapongeza Wanafunzi wa Chuo Cha Elimu ya Biashara (CBE) ambao wamefanya vizuri zaidi katika fani mbalimbali.

Sambamba na tukio hilo Mgeni Rasmi Bi. Stella Kahwa alitembelea mabanda yaliyoandaliwa kuonesha bunifu mbalimbali za Wanafunzi wa Chuo Cha CBE ambapo ameupongeza Uongozi wa CBE kwa kuwalea vyema Wanafunzi na kusimamia bunifu zao.

Bi. Stella ameeleza kuwa kwa sasa nchi inahitaji vijana wabunifu ambao wataweza kuchukua nadharia za darasani na kuziweka katika vitendo kama inavyotakiwa.

Kadhalika, Mgeni Rasmi Bi. Stella Kahwa amefurahishwa kuona bidhaa zinazozalishwa na Wanafunzi hao zimefungashwa kwa kuzingatia Vipimo sahihi na ameupongeza pia ubunifu ulioandaliwa na Wanafunzi wanaosoma kozi ya Vipimo ambao umelenga kurahisisha Upimaji wa matenki makubwa kwa njia za kisasa zaidi na ameahidi WMA itakutana nao na kuona namna ya kuboresha ubunifu huo kwani utasaidia sana.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo Cha CBE Prof. Tandi Lwoga amesema katika kuendeleza taaluma, utafiti na ushauri wa kitaalamu CBE inashirikiana na sekta mbalimbali za binafsi na Serikali na hivi karibuni CBE na WMA zimesaini makubaliano ya Wanafunzi wa kozi ya Vipimo kusoma darasani kwa muda wa mwaka Mmoja na nusu na mwaka Mmoja na nusu mwingine kusoma kwa vitendo wakifanya kazi ambapo itasaidia kuzalisha wataalamu wenye uelewa zaidi na kazi zinazoenda kufanyika.